Jumanne, 18 Desemba 2018
isimujamii
SOMO LA KWANZA
ISIMUJAMII
1.0 Utangulizi
Katika somo hili tutatoa maana ya isimujamii pamoja na kueleza historia yake.
Tutaeleza mikabala mbalimbali ya isimujamii. Vile vile tutaeleza uhusiano uliopo
kati ya lugha na jamii. Aidha, tutaonyesha uhusiano wa isimujamii na taaluma
nyingine. Na mwisho tutajadili mitazamo mbalimbali kuhusiana na swala la
lugha.
1.1 Madhumuni
Baada ya kulipitia somo hili, tunatarajia kwamba utaweza:
i. Kutoa maana kamili ya isimujamii pamoja na kueleza historia yake.
ii. Kueleza kikamilifu mikabala ya isimujamii.
iii. Kuonyesha uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii.
iv. Kueleza uhusiano wa isimujamii na taaluma nyingine.
1.2 Isimujamii ni nini?
Wataalamu wametoa fasiri mbalimbali za neno isimujamii . Labov (1992:183)
anaeleza kuwa, isimujamii ni mtazamo wa kiutafiti wa isimu unaolenga
matumizi ya lugha katika jumuia lugha . Pride (1972:287) anasema kuwa
isimujamii ni uchunguzi wa lugha kama sehemu ya utamaduni na jamii . Lyons
(1981) anaiainisha isimujamii kama tawi moja muhimu la isimumakro
(microlinguistics), matawi mengine yakiwa isimunafsia, isimuethnolojia, n.k.
Hudson (1980:1) anaieleza isimujamii kuwa ni, uchunguzi wa jinsi lugha
inavyohusiana na jamii .
Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa isimujamii ni taaluma inayochunguza lugha
kama inavyotumiwa na jamii katika fani na mazingira mbalimbali ya kila siku.
5
Mkazo katika isimujamii umewekwa kwa watumiaji wa lugha wenyewe. Basi
isimujamii ni taaluma ambayo inapanua mawanda ya kimuktadha ya isimu kupita
yale mazungumzo.
KUMBUKA
Isimu jamii imejumuisha maneno mawili: Isimu na jamii.
Isimu ni sayansi ya lugha.
Jamii ni mkusanyiko wa vitu vinavyofana.
1.2.1 Isimu jamii inahusu nini?
Wardhaugh (1986} anasema kuwa isimujamii inahusika na uchunguzi wa kuweka
wazi uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii ikiwa na lengo la kuelewa muundo
wa lugha na jinsi lugha inavyofanya kazi katika mawasiliano. Katika isimujamii
tunaichunguza jamii ili kufahamu mengi zaidi kuhusu lugha.
Labov (1980) aneleza kuwa eneo jingine la utafiti ambalo limeongezwa katika
isimujamii ni sosholojia ya lugha. Hii hushughulika na maswala mengi ya
kijamii na jinsi yanavyoingiliana na lugha na lahaja. Haya ni pamoja na matatizo
yanayohusishwa na kudhoofika na hata kufa kwa lugha na kumezwa kwa lugha
zenye watu wachache, maendeleo ya uwili-lugha, usanifishaji wa lugha, na
upangaji wa lugha hasa katika mataifa yanayoendelea.
Eneo lingine ambalo linajumuishwa katika isimujamii na linahusika na lugha
katika matumizi yake ni ethnografia ya mawsiliano. Ethnografia ni maelezo
ya kisayansi kuhusu mbari, mila, utamaduni wa binadamu. Mambo yanayohusika
hapa ni kueleza na kuchanganua ruwaza za matumizi ya lugha na lahaja katika
utamaduni fulani: matukio yanayozusha mazungumzo, uhusiano kati ya
mzungumzaji, hadhira, mada, njia ya kuwasilisha na muktadha. Pia katika
isimujamii kuna sajili au rejista ambayo hurejelea matumizi tofauti tofauti ya
lugha.
6
Pamoja na hayo kuna kuchanganya lugha tofauti hivi kwamba tunapata kubadili
msimbo (code switching) na kukopa, na jinsi lugha tofauti zinavyoingiliana
hata kusababisha pijini na krioli.
Hudson (1984:4-5) anasema kuwa, isimujamii hushughulikia wazungumzaji
binafsi kama wanachama wa makundi ya kijamii na huuliza maswali kama vile,
kwa nini kuna tofauti nyingi kati ya makundi haya, na tofauti hizo ni zipi .
1.3 Historia Fupi ya Isimujamii
Katika miaka 50 hivi iliyopita, utambuzi wa umuhimu wa uhusiano kati ya lugha
na jamii umepelekea kukua kwa taaluma mpya inayoitwa isimujamii. Ingawa
kulikuwa na haja ya kuichanganua lugha kulingana na miktadha yake ya
matumizi katikati mwa karne iliyopita, jina la isimujamii halikutumika hadi
mwaka wa 1952 katika kazi ya Haver C. Currie, aliyekuwa Mshairi na
Mwanafalsafa (Tazama Mesthrie (2001). Miaka kumi baadaye istilahi
sociolinguistika ilitumika Urusi, na katika mwaka wa 1964 utafiti wa isimujamii
ukasambaa Marekani.
Isimujamii kama taaluma imekua na kupata maendeleo makubwa katika miaka
ya mwishoni mwa sitini (1960 s) na mwanzoni mwa sabini (1970 s). Hata hivyo
uchunguzi ulioihusisha lugha na jamii umekuwepo tangu zamani hasa wataalamu
walipochunguza lahaja na uhusiano kati ya maana ya maneno na utamaduni.
Kongamano la kwanza la isimujamii lilifanyika katika Chuo cha University of
California- Los Angeles mwaka wa 1964. Huu ndio mwaka ambao isimujamii
imejitokeza kikamilifu kama taaluma. Tangu hapo utafiti mwingi umefanywa na
waandishi mashuhuri wa taaluma hii miongoni mwao wakiwa, Grimshaw, Hymes,
Fishman, Gumperz, Labov, na Lieberson. Taaluma hii imejulikana pia kama
sosholojia ya lugha.
7
1.4 Mikabala ya Isimu Jamii
Kama tulivyosema hapo mwanzoni, wanaisimujamii hawafasiri isimujamii kwa
namna moja. Zipo sababu nyingi za kutofanya hivyo, lakini tutatoa tatu tu:
(a) Sababu ya kwanza inatokana na fasiri ya lugha. Wapo wanaisimu
wachache kama vile Labov 1972, Trudgill 1974, Halliday and Martin 1981
n.k ambao bado wanaichambua lugha ya jamii kwa kufuata misingi ya
kiisimu.
(b) Wataalamu waliofafanua isimujamii, walilielewa neno jamii kwa namna
tofauti. Baadhi walishikilia maana pana ya kuhusisha watu wote waishio
katika taifa moja (lenye makabila na mataifa mbalimbali pamoja).
Wengine wamechukua maana finyu ya kuhusisha wale watu waishio
katika sehemu moja walio na lugha moja na kuchangia utamaduni mmoja.
(c) Pia kumekuwepo na misisitizo mbalimbali katika ufafanuzi wa isimujamii.
Wapo wanaisimu wanaoelezea lugha ya jamii kwa kufuata mwelekeo wa
kisaikolojia, kisosiolojia, kianthropolojia, kihistoria, kiethnolojia, nk.
Kwa sababu hii kumetokea mikabala mitatu ya isimujamii:
(a) Mkabala wa kimaikro
(b) Mkabala wa kimakro
(c) Mkabala kati
1.4.1 Mkabala wa Kimaikro
Mkabala wa kimaikro unajumuisha mitazamo yote ambayo inafafanua isimujamii
kwa kufuata mbinu na nadharia za kiisimu. Mkabala huu hutazama isimujamii
kama mwendelezo wa taaluma ya isimu.
Je, ni nini mawanda ya isimujamii kwa mujibu wa mkabala huu? Si rahisi
kusema kwa mkato kuwa mawanda ya isimujamii yanaanza hapa na kuishia pale.
8
Tunachoweza kusema ni kuwa wakati uchambuzi wa kiisimu unatilia mkazo
maana itokanayo na kuchunguza uhusiano wa maneno kiwima na kiusilisila
(syntagmatic uhusiano wa kiulalo wa vipashio vya tungo) katika sentensi,
uchambuzi wa kupata maana kiisimujamii unaongezea juu yake sifa za kijamii.
Kwa mfano:
(i) Amekwenda ntoni kuchota maji
(ii) Mtoto ayupo apa
Katika mifano hii, mtaalamu wa isimu atakuwa na haya ya kusema.
1. Atagundua kwamba mwandishi ametumia maneno ntoni , ayupo , apa
badala ya mtoni , hayupo na hapa . Katika ufafanuzi wake atasema kuwa
hayo si maneno sanifu ya Kiswahili ni maneno yatokanayo na lugha
mbalimbali. Ataeleza ni kina nani wanazungumza lugha ya Kiswahili hivyo.
2. Licha ya kasoro za matumizi ya maneno hayo, sentensi zote mbili zinatoa
maana zilizokusudiwa. Katika sentensi ya kwanza tunafahamu kuwa mtajwa
hakwenda mahali pengine isipokuwa mtoni kwa madhumuni ya kuchota maji.
Sentensi ya pili ina maana kuwa mtu ambaye hayupo ni mtoto wala si mtu wa
rika jingine. Tunazipata maana kwa kuzingatia uhusiano wa maneno kama
yalivyotumika katika sentensi.
Mwanaisimu jamii atazichambuaje sentensi hizo hapo juu?
Kwanza, atakubaliana na uchambuzi uliofanywa hapo juu pamoja na maana
zake.
Pili, atataka kujua watu gani (wa sehemu gani [kabila], umri gani, kisomo
gani, kipato kipi, wake au waume) wanaotamka ntoni , ayupo na apa
badala ya mtoni, hayupo na hapa.
Tatu, atataka kujua sababu zinazowafanya watamke hivyo.
Nne, atataka pia kujua ni wakati gani na katika mazingira gani mtu hutamka
hivyo. Inawezekana wanatamka hivyo wanapoongea na watu wa makabila
yao lakini wanayatamka vizuri wanapoongea na watu wa makabila tofauti.
Uchambuzi wa Kiisimujamii unatuonyesha mambo kadha wa kadha ya
9
kimsingi:
Baadhi ya maneno (ntoni, ayupo na apa) yaliyotumika katika sentensi zetu
yanahusishwa na aina mbalimbali za watu katika jamii. Hii ina maana
kuwa lugha si tu kuelewa maana ya maneno bali pia hutumika kuielewa
jamii ilivyo.
Pili, hatuwezi kudai kuwa mtu anayetumia maneno ya vilugha katika
mazungumzo yake hajui kutamka maneno ya Kiswahili sanifu. Mtu
anaweza kutumia vilugha kwa sababu zake mbalimbali ikiwemo ile ya
kutaka kuonyesha mshikamano wake na watu wa kabila lake au watu
watokao sehemu moja kihistoria na kijiografia.
Miongoni mwa wafuasi wa mkabala huu ni pamoja na Labov (1972) na Trudgill
(1974). Labov (1972) amejitokeza kuwa mwanaisimu mashuhuri katika miaka ya
sabini (1970) kutokana na utafiti wake ulioonyesha uwezekano wa kuoanisha
alama za kiisimu (linguisitic forms) na zile za kijamii na kufanikiwa kupata habari
zaidi juu ya jamii hiyo.
Labov aliufanya utafiti mjini New York ulioonyesha kuwa watu wa tabaka la chini
hutamka sauti (r) inayosikika katika kuyatamka maneno yenye fonimu /r/ kuliko
watu wa matabaka mengine. Labov anatumia nadharia na mbinu zile zile za
isimu kuelezea isimu jamii. Pia anachunguza ni mazingira yapi na sababu zipi
(kiisimu/kijamii) zinazoleta ubainifu miongoni mwa watumiaji wa lugha.
1.4.2 Mkabala wa Kimakro
Huu ni mkabala unaoangalia isimujamii kinyume na mkabala wa kimaikro. Ni
mkabala wa kimakro kwa sababu unahusisha watu wengi kijiografia. Mkabala
huu unaeleza na kufafanua lugha kwa kutumia mwingiliano wa mbinu na dhana
mbalimbali kutoka taaluma nyingine za kijamii. Mkabala huu huangalia mambo
yote yanayohusu utumiaji wa lugha kwa ujumla katika jamii. Kujua lugha
10
zilizopo katika jamii na uhusiano wake na lugha nyingine ni moja tu ya mambo
ya kimsingi ya mkabala huu.
Kwa mfano, mwanaisimu jamii wa mkabala huu, hupenda kujua sababu za
msingi zinazofanya lugha moja iteuliwe kuwa lugha ya taifa, lugha rasmi, au
lugha ya kufundishia katika elimu. Sababu kama hizo aghalabu huwa hazina
budi zitokane na misingi ya pamoja ya kiisimu na kijamii. Pia, hata zile lugha
ambazo hazikuteuliwa kuchukua dhima fulani kitaifa, bado kwa mujibu wa
mkabala huu lugha hizo ni muhimu kukuzwa na jamii zinazohusika ili
kuziimarisha. Nani anazungumza lugha ipi, wapi, kwa nini, na kwa madhumuni
gani, ni miongoni mwa maswala muhimu yanayoshughulikiwa na mkabala huu.
Mwanaisimujamii haangalii maana ya tamko peke yake bali huangalia maana kwa
kuzingatia taratibu na kanuni za mawasiliano zinazotumika katika jamii
inayohusika. Hii ina maana kwamba, uchambuzi wa kupata maana katika lugha
haufanywi nje ya taratibu za kijamii na mazingira ya tamko lenyewe. Neno
mazingira hapa lina maana ya kuhusisha mahali tamko liliposemwa, kujua
habari za mzungumzaji na msikilizaji pamoja na uhusiano wao na kujua taratibu
na kanuni zinazotawala mawasiliano ya lugha inayohusika.
Mkabala huu hauchambui sentensi zisizotumiwa katika mazungumzo ya
majibizano. Ni katika msingi huu ndipo sentensi:
(i) Amekwenda ntoni kuchota maji.
(ii) Mtoto ayupo apa.
haziwezi kutupatia uchambuzi unaoridhisha kwa mujibu wa mkabala huu.
Tunahitaji kuchambua sentensi au matamko yatokanayo na mazungumzo na
majibizano kama mfano wetu hapa chini unavyoonyesha:
(iii) Baba Mkwe: Mwanangu, umefika salama?
(iv) Mkwe: Ndiyo baba, tumefika salama.
(v) Mkwe: Haya baba, mfike salama.
11
(vi) Baba Mkwe: Asante Mwanangu.
Katika kuchambua maana za sentensi hizi uhusiano wa mzungumzaji na
msikilizaji ni muhimu sana kuzingatiwa. Uchambuzi unatuonyesha kuwa katika
sentensi (iv) mkwe ametumia kiambishi cha wingi tu badala ya umoja. Vile vile
katika sentensi (v). Je, tunaweza kusema kuwa huyu mkwe hajui matumizi
sahihi ya viambishi nafsi?
Hapa, maswala kama ya utamaduni, kaida na kanuni za mawasiliano katika jamii
n.k. yanafaa kuzingatiwa katika uchambuzi. Kwa mujibu wa kanuni za
mawasiliano ya jamii hiyo, mtu aliye mdogo katika umri hutakiwa kutumia
kiambishi cha nafsi ya kwanza wingi badala ya umoja anapozungumza na mtu
wa umri mkubwa kama dalili ya kuonyesha heshima. Tumefikia maana hii baada
ya kuzingatia taratibu na kaida zinazotumiwa katika mawasiliano ya lugha
inayohusika.
Fishman(1972) amesema kuwa ni muhimu kwa wataalamu wa lugha kutumia
mbinu za pamoja (kiisimu na kijamii) katika kufikia uteuzi wa lugha ili zichukue
dhima mbalimbali katika jamii.
Zoezi
Je, unaweza kuonyesha tofauti kati ya isimu kimaikro na isimu kimakro kwa
kutumia mifano kutoka kwa jamii yako?
1.4.3 Mkabala Kati
Kimsingi, mkabala huu unazingatia yale mambo ya kimsingi tu kutokana na
mikabala yote miwili. Kudai kuwa lugha ielezwe na kufafanuliwa kwa kufuata
kanuni za kiisimu peke yake, ni dai la kiwango cha juu. Lakini mkabala wa
12
kimaikro bado una mambo yake ya kimsingi ambayo yanaweza kuchukuliwa na
kutumiwa katika kueleza lugha kiisimujamii. Kwa mfano, baadhi ya kanuni za
fonolojia na mofolojia zinaweza kutumiwa sambamba na sifa nyingine za kijamii
ili kueleza kaida zinazofuatwa na watumiaji wa lugha katika mazingira
mbalimbali.
Mwanaisimujamii anao uhuru wa kushughulikia uchambuzi wa lugha kwa
viwango na idadi ya watu (watumiaji wa lugha) apendao mwenyewe kulingana
na lengo la kazi yake.
Ervin Tripp (1971) ni miongoni mwa wanaisimujamii wachache wanaofuata
mkabala wa kati. Anasisitiza umuhimu wa kuchunguza kanuni za kijamii
zinazotawala mazungumzo mbalimbali ya kila siku. Anadai kuwa mazungumzo
yanayofanywa na watu hayafanywi kiholela bali hufuata kanuni za mawasiliano
katika jamii zinazohusika. Kwa mujibu wa mtazamo huu, isimujamii inapaswa
kushughulikia uchunguzi wa kanuni na kawaida za kijamii zinazotawala
mawasiliano kwa jumla.
Tumeona kuwa isimujamii ni taaluma pana na inayovuka mipaka ya isimu na
kuhusisha taaluma nyingine za kijamii. Si rahisi kuweza kueleza mipaka kati ya
isimu na isimujamii. Hii ni kwa sababu taaluma hizi zinaingiliana sana.
Mwanaisimujamii hashughuliki na utoaji wa maamuzi yahusiyo lugha kwa niaba
ya jamii. Kazi ya mwanaisimujamii ni kueleza na kufafanua lugha kwa misingi ya
isimujamii. Utoaji wa maamuzi yahusuyo lugha yameachiwa watumiaji wa lugha
wenyewe.
Swali
Ukizingatia kila mkabala, onyesha jinsi lugha inavyotumiwa katika jamii yako.
13
1.5 Lugha na Jamii
Isimujamii ni dhana ambayo imetokana na isimu na inaingtia lugha kama
inavyotumiwa katika jamii. Lugha si kifaa tu cha kuwasilisha habari bali ni
namna muhimu ya kuanzisha na kudumisha uhusiano miongoni mwa watu.
Kila tunapozungumza, wasikilizaji wetu hupata habari fulani kuhusu sehemu
tunazotoka na sisi ni watu wa aina gani. Hata mielekeo yetu na mawazo yetu
vinaweza kutumiwa na wengine kutuelewa zaidi. Mambo mawili haya ni muhimu
sana kutokana na mtazamo wa kijamii.
(a) Dhima ya lugha ya kuanzisha mahusiano ya kijamii.
(b) Dhima ya lugha ya kuwasilisha habari fulani kuhusu mzungumzaji.
Kiisimu, lugha sanifu haichukuliwi kuwa bora kuliko lahaja au lugha nyinginezo.
Lugha zote zina mifumo tata yenye kanuni za kipekee. Kule kusema kuwa lugha
moja ni bora kuliko nyingine ni jambo la kijamii, si la kiisimu. Ikiwa watu ni
maskini au wa ngazi ya chini, basi hata lugha zao zitadharauliwa. Kwa hivyo
mielekeo yetu kuhusu vilugha hivi huonyesha muundo wa kijamii wa watu.
Katika kuonyesha uhusiano uliopo baina ya lugha na jamii, wataalamu wengi
wamezungumzia nadharia tete ya Sapir-Whorf (Edward Sapir na Benjamin Lee
Whorf). Nadharia hii inaeleza kuwa lugha asilia ya mtu hutawala jinsi
anavyouelewa ulimwengu. Hii ina maana kwamba tofauti za kiisimu huweza
kuzusha utambuzi unaotofautiana. Ina maana kwamba hatuwezi kuwaza bila
lugha. Basi ikiwa mtu anaweza kudhibiti lugha wanayojifunza watu, atakuwa na
uwezo wa kudhibiti mawazo yao.
Kulingana na Sapir-Whorf (1956), binadamu huelewa mazingira kupitia kwa
lugha wanayoitumia. Wanatoa mfano wa Waeskimo ambao wana maneno
14
mengi yanayoelezea hali mbalimbali za theluji, huku Kiingereza kikiwa na neno
moja tu snow. Pia katika jamii ya Hopi, lugha yao inataja vitu kama mawingu
na mawe kama vitu vilivyo hai. Hali hii inawafanya waufikirie ulimwengu kwa
njia tofauti na watu wengine.
Eneo analoishi mtu hujitokeza katika lugha yake hasa katika muundo wa
msamiati. Kwa mfano, mfumo wa aila katika jamii hujitokeza katika msamiati wa
aila kama vile mtoto, binti, babu, nyanya, shangazi, n.k.
Pia maadili ya jamii yanaweza kuwa na athari katika lugha ya jamii hiyo. Haya
hutokea kupitia kwa miiko. Miiko huhusika na tabia ambazo zimekatazwa katika
jamii fulani. Katika lugha, miiko inahusishwa na vitu au maneno yasiyotumika au
kutajwa. Maneno ambayo ni mwiko katika lugha fulani hutuonyesha (kwa kiasi
fulani) mfumo wa maadili na imani za jamii hiyo.
Kwa hivyo mwiko ni swala la kiisimu kama lilivyo la kijamii. Miiko husababisha
maneno fulani kupotea kutoka kwenye lugha na mengine kuzuka.
Kwa hivyo, isimujamii ni sehemu ya isimu inayoiangalia lugha kama sehemu ya
kijamii na utamaduni wa watu. Inachunguza nyanja za lugha na jamii, na ina
uhusiano wa karibu na taaluma nyingine kama anthropolojia, sosholojia,
saikolojia na hata jiografia.
1.6 Isimujamii na Taaluma Nyingine
Si watafiti wa isimu na isimujamii pekee wanaohusika na uchunguzi wa lugha
katika jamii. Wataalamu kutoka kwa taaluma nyingine kama vile
wanaanthropolojia, wanasaikolojia, n.k huhusika pia.
15
1.61 Isimujamii na Saikolojia
Taaluma hizi mbili hushughulikia swala la mielekeo (attitudes) kuhusu aina fulani
za lugha. Ingawa wanaisimujamii wanachunguza kwa kina swala la mielekeo
kuhusu lugha, hili ni jambo la kisaikolojia kwa kuwa lipo katika akili ya mtu.
Uchunguzi huu ni muhimu katika kueleza mabadiliko ya kiisimu yanayojitokeza
katika lugha. Mara nyingi sababu hii hutumiwa kueleza kwa nini lahaja
inabadilika, lini na jinsi inavyobadilika. Kwa mfano, nchini Kenya vijana
wanatamka neno best kama beshte ili kuafikiana na mielekeo ya vijana kuhusu
matamshi ya maneno fulani hasa mijini.
Wanasaikolojia hutueleza jinsi mtoto anavyojifunza lugha kupitia kwa uwezo
maalum anaozaliwa nao (innate capacity), lakini pia lazima tufahamu jinsi tofauti
za kimazungumzo (mf kijinsia) zinavyokuzwa katika mchakato wa kuingiliana
kijamii.
1.6.2 Isimujamii na Anthropolojia
Anthropolojia ni taaluma inayohusika na elimu ya binadamu, hususan elimu
inayohusu habari za asili na maendeleo yake ya awali. Inachukuliwa kuwa jinsi
binadamu huyu alivyokua katika kikundi, alikuwa anazungumza lugha fulani.
Wanaanthropolojia kadha wamefanya utafiti ambao una misingi ya kiisimujamii,
kwa mfano, kwa kuchunguza mfumo wa aila wa jamii. Tunajua kuwa mfumo wa
aila hujitokeza katika msamiati. Kwa mfano, utaona kuwa jamii nyingi za Kiafrika
zina msamiati mpana unaoelezea uhusiano wa kiaila kuliko lugha za Wazungu.
Jambo hili linatueleza mengi kuhusu jamii hizo. Kwa mfano, lugha ya Kiingereza
huzungumzia aina moja tu ya shangazi (aunt) lakini katika lugha nyingi za
Kiafrika kuna maneno ya uhusiano huu kwa upande wa baba na wa mama.
Zoezi
Taja majina ya kiaila katika jamii yako na ulinganishe na ya Kiingereza.
16
1.6.3 Isimujamii na Elimu
Wanaelimu wanatakiwa kutoa maamuzi kuhusu maswala yanayohusu lugha
kama vile ufundishaji wa lugha sanifu. Wanaisimujamii wamekuwa wakijaribu
kushawishi wanaelimu wabadili mielekeo yao kuhusu lugha fulani
zinazozungumzwa na watoto fulani shuleni kama vile lugha zao za kwanza.
Wapangaji lugha huhitajika kuwa na ufahamu fulani wa kiisimu ili waweze kutoa
uamuzi unaofaa kuhusu aina ya lugha inayotakiwa kukuzwa na kuhimizwa katika
miktadha fulani, daraja na shule nk.
1.6.4Isimujamii na Utamaduni
Wanaanthropolojia hushughulikia utamaduni ili kuweza kueleza tabia za watu za
kiisimu; wanaisimujamii huoanisha lugha na utamaduni kwa kuzingatia sarufi.
Uhusiano kati ya taaluma hizi mbili unatokana na ile haja ya kuyaelewa makundi
mbalimbali ya watu. Hivi ni kusema kwamba ni vigumu kwa wanaanthropolojia
kuchunguza jamii za kale bila kuzingatia lugha za watu hao; na pia ni vigumu
kuchunguza lugha bila kuzingatia uamilifu wa mazungumzo fulani katika jamii.
Kwa kuzingatia lugha, maana ya ujumbe fulani ni kile kitu ambacho
kimewasilishwa kila wakati mwanajamii anapoongea. Na tukizingatia tabia za
kijamii, maana ni kile kitu ambacho kimewasilishwa wakati mwanajamii fulani
ametenda (kitu fulani) kitendo cha kitamaduni. Kwa hivyo lugha na utamaduni
ni tabia za binadamu. Mtazamo wa kipragmatiki hutupa zaidi ya ile maana ya
maneno.Unaangalia pia vikwazo vya kijamii anavyokabiliana navyo mtumiaji
lugha, na athari nyinginezo za kijamii katika matumizi ya lugha. Lazima pia
tuzingatie muktadha wa maongezi ili tuielewe kauli fulani.
17
1.6.5 Isimu na Sosholojia (Elimujamii)
Wanaisimujamii hutalii miundo ya kijamii na namna miundo hiyo inavyoathiri
lugha. Kuna nguvu fulani za kijamii ambazo husababisha wanajamii kutaka
kuongea au kutamka maneno kwa njia fulani. Mkondo unaochukuliwa na
kibadala (variant) fulani cha kiisimu katika jamii si jambo linalojitokeza kiholela
tu, bali ni kitu kinachotokana na tathmini za kijamii. Uchaguzi wa kipashio fulani
cha kiisimu unatokana na jinsi jamii inavyochukulia kipashio hicho. Lugha
hutueleza mengi kuhusu mtu katika jamii.
Kumbuka
Kwa sababu isimu-jamii ni taaluma inayohusika na jamii moja kwa moja,
Ina uwezo wa kuhusiana na taaluma nyingi sana.
1.7 Mitazamo ya Lugha
Wanazuoni mbalimbali wakiwemo Greenberg (1957), Hymes (1974), Dik (1978)
nk wanaiangalia lugha kwa mitazamo miwili: mtazamo wa kiisimu na ule wa
kiisimujamii.
Katika mtazamo wa kwanza (wa kiisimu), lugha inaelezwa kuwa ni mfumo wa
sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana
ili kuwasiliana. Mtazamo huu unachukulia lugha kuwa kitu halisi ambacho
kinaweza kuainishwa katika vipande sauti vidogo vidogo ambavyo kwa pamoja
huunda mfumo wa lugha wa mawasiliano.
Chomsky (1957) aliunga mkono mtazamo huu. Katika kuifafanua lugha,
alitofautisha hali ya umilisi na utendaji. Umilisi ni kile ambacho mzungumzaji
anafahamu kuhusu lugha yake. Uwezo huu humwezesha kuelewa na kutoa
sentensi nyingi jinsi anavyotaka kuwasiliana. Huku ni kufahamu kanuni
18
zinazoitawala lugha husika na uwezo huu umo akilini mwake. Utendaji ni jinsi
mzungumzaji anavyoitumia lugha.
Kutokana na maelezo haya ni kama Chomsky anatueleza kwamba tusiichunguze
lugha katika matumizi yake, au hata jinsi tunavyojifunza lugha, bila kwanza
kufahamu lugha ni nini. Anaona kuwa kazi ya mwanaisimu ni kuandika au
kutunga sarufi na kukuza uelewa wetu wa lugha.
Kuna wataalamu ambao wamepinga msimamo huu. Kwa mfano, Labov anaiona
sarufi kama mali ya kikundi/jamii au jumuia lugha na wala si mali ya kisaikolojia
ya mtu binafsi. Hudson (1980:19) anaona kuwa mtazamo wa lugha usiohusisha
jamii una upungufu. Nadharia fika ya lugha lazima itaje matumizi ya lugha
hiyo. Anasema kuwa unweza kuitenga lugha na jinsi ya kwa nini inatumiwa.
Kwa hivyo lugha ni sehemu ya jamii.
Umilisi wa kimawasiliano hauhusu tu kufahamu mfumo wa lugha, bali pia ni nini
unachosema na kwa nani, na namna utakavyokisema katika muktadha fulani.
Unashughulikia ujuzi wa kijamii na kitamaduni ambao hudhaniwa kuwa
wazungumzaji wanao unaowawezesha kufasiri mifumo ya kiisimu. Fonolojia,
sintaksia na msamiati ni sehemu tu ya vipashio vinavyotumiwa katika
mawasiliano. Pamoja na hivyo lazima kuwepo semantiki, muktadha na kwa
jumla mtazamo wa kijamii wa lugha.
Hivyo basi ufafanuzi wa Chomsky wa lugha una upungufu kwani unaichukulia
lugha kama kitu kinachojitosheleza. Unaiondoa lugha kutoka kwenye jamii.
Hapa ndipo isimujamii inapoingilia ili ilete kipengele cha jamii katika lugha.
Mtazamo wa pili wa lugha ni wa kiisimujamii. Mtazamo huu unaangalia lugha
kama sehemu ya utamaduni wa jamii ulio na ruwaza ambazo hurithishwa na
watu wenyewe kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mtazamo huu unaichukulia
19
lugha kama mali ya jamii. Wanaisimujamii wanakubaliana na fasiri hii ya pili ya
lugha.
Zoezi
Isimu jamii ni nini?
Taja mikabala mitatu ya isimujamii na uonyeshe kwa kutoa mifano jinsi
inavyoingiliana na kutofautiana.
Eleza uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii.
Isimujamii ni taaluma inayoingiliana na taaluma nyingi katika jamii.
Fafanua kauli hii.
Muhtasari
Katika somo hili, tumeeleza maana ya isimu jamii na mambo haya
yamezingatiwa;
Tumeonyesha mikabala mitatu ya isimujamii.
Tumeonyesha uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii.
Tumeonyesha jinsi isimujamii inavyoingiliana na taaluma nyingine.
Tumeeleza mitazamo miwili ya lugha kwa kuzingatia maoni ya wataalamu
mbalimbali.
20
Marejeleo Teule
Chomsky, N.(1957),Syntactic structures.The Hague. Mouton
Dik, S.C.(1978) Functional Grammar. North-Holland Linguistics Series. North-
Holland Publishing Company. New York.
Fishman, J.A. (1967) Sociolinguistics and the Language Problems of Developing
Countries katika Fishman, J.A. et.al. (eds.) Language Problems of Developing
Nations. John Wiley and Sons. Inc. London.
(1972) Domains and the Relationship between Micro and Macro
Sociolinguistics katika Gumperz, John & Dell Hymes (eds.) Directions in
Sociolinguistic:The Ethnography of communication.Basil Blackwell.oxford
Greenberg, J.H. (1957) Essays in Linguistics, Chicago: Phoenix Books.
Hudson, R. (1980) Sociolinguistics: Cambrdige, University Press, Cambridge.
Hymes, D. (1974) Foundations in Sociolinguistics: University of Pennyslavania
Press, Philadelpia.
Labov (1980) (Mhr.) Locating Language in Time and Space. Academic Press.
New York.
Mesthrie, R. et.al. (2000) Introducing Sociolinguistics. Edinburgh University
Press, Edinburgh.
Msanjila, Y.P. (1995) Mawanda ya Isimu Jamii katika Mbogo, E. na McOnyango,
O. (wahariri) Baragumu Juzuu la 2 Nam. 1 & 2 Uk. 65-71, Chuo Kikuu Maseno.
Pride, J. G. & Holmers J. (eds.) (1972) Sociolinguistics Harmondsworth:
Penguin.
Wardhaugh, R. (1992) An Introduction to Sociolinguistics. Blackwell.
Whorf, B.L. (1956), Language, Thought and Reality: Selected Writings, J.B.
Carroll (ed). Cambridge, MA:MIT press
21
SOMO LA PILI
NADHARIA ZA KIJAMII
2.0 Utangulizi
Sehemu hii inashughulika na kueleza nadharia za kijamii ambazo hutumika katika
kuelewa uhusiano mbalimbali katika jamii. Nadharia hizi zinasaidia kuelewa wazi
swala la lugha na jamii.
2.1 Madhumuni
Mnamo mwisho wa somo hili utaweza kutimiza yafuatayo:
1. Kueleza nadharia za kijamii.
2. Kuonyesha jinsi nadharia hizo zinavyoingiliana na swala
la lugha.
2.2 Nadharia za Kiisimu
Ili kuzingatia sehemu ya kijamii iliyo katika taaluma ya isimujamii, ni muhimu
kuelewa mitazamo mbalimbali inayotumiwa kuchunguza jamii za wanadamu.
Katika sosholojia kunazo nadharia tatu kuu zinazoielezea jamii. Kuelewa lugha
katika jamii kunahitaji pia kuzielewa nadharia hizi za kijamii. Katika mada hii
tutazijadili nadharia mbili za mwnzo kati ya hizi tatu. Nadharia hizo tatu ni:
(a) Uamilifu (functionalism)
(b) Umaksi (marxism)
(c) Muingiliano (interaction)
2.2.1 Uamilifu
Hii ni nadharia iliyoibuka kati ya miaka ya arobaini na sitini (1940 s and 1960 s).
Inaeleza kuwa jamii inaweza kuchukuliwa kama mfumo ulio na sehemu zenye
uamilifu. Ili kuelewa sehemu yo yote ya jamii (kama familia au shule), lazima
sehemu hiyo ichunguzwe kwa kuangalia uhusiano wake na jamii nzima. Kama
vile mwanabiolojia anavyochunguza mchango wa moyo katika kuendeleza
22
maisha ya binadamu ndivyo sehemu ya jamii inavyochunguzwa kulingana na
mchango wake katika kuendeleza mfumo wa kijamii.
Mfumo wa kijamii unayo mahitaji fulani ambayo yanahitaji kutekelezwa ili jamii
idumu. Mahitaji haya ni pamoja na chakula, mavazi na malazi. Uamilifu wa
sehemu yo yote ya jamii ni ule mchango wake katika kuendeleza na kuimarisha
jamii hiyo kwa jumla. Hii ina maana kwamba kuna kiwango fulani cha
muingiliano kati ya sehemu zote ambazo huunda jamii.
Wanauamilifu wanadai kuwa utaratibu na uimarikaji ambavyo huwa ni vitu
muhimu vya kuendeleza jamii hutokana na kuwepo kwa amali (za pamoja) sawa,
yaani makubaliano kuhusu mambo fulani katika jamii. Kutokana na mtazamo
huu wanajamii hushughulikia mifumo midogo ya kijamii na amali sawa
zinazowaunganisha wanajamii.
Dhana zinazosisitizwa katika nadharia hii ya elimujamii na ambazo ni muhimu
kwa mwanaisimu jamii ni pamoja na: utamaduni, ujamiishaji (socialisation),
kaida, amali, hadhi na majukumu/dhama.
(i) UTAMADUNI
Utmduni hurejelea jinsi jamii inavyoishi; yaani mkusanyiko wa mawazo na tabia
wanazojifunza na kupokeza kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Katika hali hii
utamaduni ni mpangilio wa jinsi watu wanavyoishi. Utamaduni unafafanua
mambo yanayokubalika na mfumo wa tabia katika jamii fulani.
(ii) UJAMIISHAJI
Dhana hii inarejelea njia ambazo kwazo watu hujifunza utamaduni wa jamii zao.
Ujamiishaji wa kimsingi au awali hutokea utotoni, aghalabu katika familia.
Mahirimu au marika (peer group) ni kukundi muhimu cha kuendeleza ujamiishaji.
Marika humsaidia kumkuza mtu kijamii na kiisimu.
23
(iii) KAIDA NA AMALI
(a) KAIDA
Kaida ni mwongozo maalumu wa jinsi ya kutenda mambo na kaida hueleza tabia
zinazokubalika na zile zinazofaa katika miktadha maalumu. Mifano ya kaida hizi
inaonekana katika mavazi ya shuleni, ya vijana,ya nyumbani, au ya dhifa
mbalimbali. Katika hali ya ujamiishaji, kaida hufunzwa kwa kutuza (kumpa mtoto
peremende, maneno ya kusifia) au kuadhibu. Baadhi ya kaida hufanywa kuwa
sheria za kutumikia umma wote. Kwa mfano, kukataza kuoga hadharani au
wanawake kuhitajika kufunika nyuso zao hadharani.
AMALI
Amali hutoa miongozo ya kijumla ya mambo ambayo yanachukuliwa kuwa
mazuri na yenye thamani. Kwa mfano, katika jamii nyingi za kisasa, watu
huthamini maisha ya binadamu sana. Baadhi ya amali zinazopendekezwa ni
umoja,uaminifu, upendo, n.k..
Wanauamilifu wanaamini kuwa ikiwa kaida hazitakubaliwa na kushirikishwa
miongoni mwa wanajamii, jamii haziwezi kushirikiana na kufanya kazi pamoja.
Hivyo basi jamii inahitaji kaida na amali za pamoja. Jambo hili limekuwa msingi
wa tafiti nyingi za isimujamii.
(iv)HADHI NA MAJUKUMU
Hadhi hurejelea cheo cha mtu katika jamii (si lazima iwe kazi). Hadhi kama hizi
huenda zimerithiwa, yaani mtu anapozaliwa anajipata ana hadhi fulani kwa
mfano malkia au mfalme. Anapoendelea kukua anajipata kuwa yeye ni mke au
mume . Hadhi pia huenda ikapatikana kutokana na juhudi za kibinafsi za mtu,
kwa mfano, kujiendeleza kitaaluma na kuwa mwalimu, daktari, mwanamichezo,
n.k.
24
Kila hadhi katika jamii huwa na idadi fulani ya kaida ambazo zinaeleza namna
mtu aliye katika hadhi hiyo anatakiwa kuendesha maisha yake. Kikundi hiki cha
kaida huitwa dhima au majukumu. Majukumu ya kijamii ndiyo huongoza
tabia. Kufikia mwisho mwa siku, mtu huwa ametekeleza majukumu mbalimbali:
mwalimu (kazini), mama au mke (nyumbani), mteja (benki), manju (kilabu cha
starehe), n.k. Kila jukumu huhitaji tabia fulani zizingatiwe, zikiwa ni pamoja na
tabia za kiisimu. Kila jukumu la kijamii humfanya mtu achague elementi fulani za
kiisimu. Huku akitekeleza majukumu yake atatumia lugha kwa njia tofauti
tofauti.
Zoezi
Je, kwa maoni yako, unafikiri nadharia ya uamilif inajitokeza vipi katika jamii
zetu na lugha tunazozitumia?
2.2.2 UMAKSI
Umaksi unahusiana na nadharia kadhaa. Tunapoongea kuhusu uhakiki wa ki-
maksi, huwa tunairejelea mikabala mbalimbali ambayo misingi yake ni mawazo
yanayohusishwa na Karl Marx na Friedrich Engels.
Nadharia hii imepitia mabadiliko makubwa tangu kuweko kwa wataalamu hawa.
Umaksi unahusu nyanja mbalimbali kama uchumi, historia, jamii na mapinduzi.
Umaksi una sifa ya kijumla inayojitokeza katika mwelekeo wake wa kuligusia kila
eneo, na kuwa na la kusema kuhusu takriban kila kitu ikiwemo lugha.
Mawazo ya Karl Marx kuhusu historia na miundo ya kijamii yana nafasi kubwa
katika nadharia hii. Umaksi ni falsafa yakinifu hasa kwa kuwa pana msisitizo
mkubwa kwenye msingi wa hali za kiyakinifu za maisha kama mazingira ya kuishi
kuliko mawazo katika maisha ya binadamu. Umaksi hauegemezi mfumo wake wa
25
kifalsafa kwenye dhana dhahania kama urembo, ukweli au ndoto bali
unayaegemeza kwenye uhalisi unaoonekana.
Hebu basi tuchunguze mawazo ya kimsingi ya nadharia hii:
(1) Historia ya maisha ya binadamu inaweza kuelezeka katika misingi yakinifu
ya kiuchumi. Misingi hii itachunguza njia za uzalishaji mali pamoja na
miundo ya kiuchumi inayoathiri sio uzalishaji mali hiyo tu bali na
usambazaji wake. Swala hili la uzalishaji mali na usambazaji wa mali hiyo
linaunda kile ambacho hujulikana kama msingi au muundo msingi (base =
infrastructure). Kwenye msingi huo ndiko kunakoegemezwa muundo wa
juu au kikorombwezo (superstructure). Muundo wa juu ndio unaohusisha
maadili, itikadi, dini, utamaduni ,n.k.
Sifa za muundo juu zinaathiriwa kwa kiasi kikubwa na muundo msingi.
Hata hivyo mabadiliko yanayotokea katika muundo wa juu kama mageuzi
katika muundo wa kiutawala huweza kuathiri muundo msingi.
(2) Daima historia ya binadamu itadhihirisha au kuakisi harakati
zinazoendelea katika matabaka ya kiuchumi-jamii. Karl Maksi aliwahi
kusema kuwa historia ya maisha ya binadamu ni ya harakati za kitabaka.
Je, harakati hizi zinasababishwa na nini? Tunajua kuwa kitu cha msingi
katika maisha ya binadamu ni kula na kunywa, kupata malazi na mavazi
na mambo mengine.
Tendo la kwanza la kihistoria kwa hiyo, ni kutafuta njia ya kuyakidhi
mahitaji haya ya kimsingi. Ili kufanikiwa katika lengo hilo, binadamu
hulazimika kujiunga pamoja au kuunda umoja ili kuimarisha ubora na
wepesi wa kuizalisha mali ya kukidhi mahitaji hayo. Muungano huo huwa
na ugawaji wa majukumu au kazi ambayo ndiyo msingi wa kuundwa kwa
matabaka katika jamii. Hatua ya juu ya mwendeleo huu ni ukuzaji wa
mfumo wa ubepari. Katika mfumo huu, mali inamilikiwa na idadi ndogo
26
ya watu. Watu hao wanaipata mali yao kutokana na unyonyaji wa umma
na hasa wafanya kazi.
Kumbuka
Zingatia maoni haya katika muktadha wa lugha. Kwa mfano lugha-
wenyeji na lugha za kigeni zilizopo hapa nchini.
Kadiri mfumo wa ubepari unavyoendelea ndivyo ubora wa uzalishaji maji
unavyoongezeka na tofauti kati ya matabaka kuimarika kwa kuwa kuna watu
wanaofaidika kwa njia zisizo za haki. Kufaidika huko kwa njia zisizo za haki,
pamoja na mbegu za kujiangamiza zilizomo kwenye mfumo wa ubepari
vinachangia kuuangusho mfumo wenyewe. Marx anaamini kuwa haya
yanatokana na mfanyiko wa kiasilia wa kihistoria. Mfanyiko huo ni wa kipembuzi
(dialectics). Kwa mujibu wa mawazo haya, historia huendelea kutokana na
mfululizosafu wa mkinzano wa mawazo. Matokeo ya mkinzano huo ni kuzuka
kwa hatua nyingine mpya ya kihistoria. Huu ndio msingi wa kile kinachoitwa
upembuzi wa kiyakinifu (dialectical materialism).
(3) Matamanio na matakwa yaliyopo katika jamii na hasa tabaka lenye nguvu
yanaakisiwa katika itikadi iliyopo katika jamii, jinsi na miundo ya mawazo
ambayo aghalabu huwa imeshika kwa nguvu na huwapo kila mahala kiasi cha
kuwa huenda wanajamii wasiitambue kwa haraka.
(4) Njia ya kusaidia na labda hata kuharakisha kuangamizwa kwa mfumo wa
kibepari ni kudadisi, kukosoa, kushutumu, kulaumu na kufichua batili iliyopo
katika itikadi ya kibwanyenye inayooimarisha ubepari.
Dhana za kimsingi zimeibuka katika nadharia hii: ukengeushi; ubidhaaishaji na
itikadi.
27
(i) Ukengeushi (alienation): Ugawaji wa kazi unaishia kusababisha utengano
fulani kati ya wanaohusika au binadamu. Hii ni hatua ya kimsingi ya
ukengeushi . Mfumo wa kibepari unapoendelea kuboreka unasababisha hali
ambapo uhusiano uliopo kati ya mfanya-kazi na tokeo la nguvu zake ni wa kitu
kigeni (alien object). Watu wanaishia kukengeushwa na jamii yao kutokana na
mfumo wa kiainisho (specialization) unaosisitizwa na kukuzwa na ubepari.
(ii) Ubidhaaishaji: Maksi anaitumia dhana ya bidhaa kukieleza au kukirejelea
kitu kinachozalishwa sio kwa nia ya kutumiwa bali kubadilishwa katika mfumo wa
kibepari wa soko. Bidhaa hizo hazitathaminiwi kutokana na kazi yake bali ni
kutokana na bei zinazoweza kuvuta. Yaani msingi wa kuzitathmini sio thamani
kimatumizi bali ni thamani kimabadilishano. Katika msingi huu, bidhaa zinaishia
kuhusisha nguvu au kanuni fulani fiche ambazo huwavuta watu na kuwafanya
wawe na mvuto mkubwa wa kukimiliki kitu fulani ambacho kinawasisimua. Huu
ndio msingi wa kuabudu bidhaa (fetishism of commodities).
Hii ni sifa kuu katika mfumo wa kibepari na ni msingi wa uchumi wa kibidhaa
ambapo watu husukumwa na kani za kununua na kumiliki vitu ambavyo labda
hawavihitaji au wanavikinai haraka na kutamani vingine. Sifa hii ya ubidhaaishaji
inaishia kuwahusu binadamu ambao hawathaminiwi kama binadamu ila kutokana
na uwezo wao wa kuzalisha mali.
(iii) Itikadi: Ni dhana telezi, lakini kimsingi ni uwasilishi wa pamoja wa mawazo,
fikira na tajriba hasa ikiwa vitalinganuliwa na uhalisia wa kiyakinifu
vinakoegemezwa. Dhana hii inaweza kufafanuliwa katika muktadha wa lugha
pale ambapo watu wanaamini kuwa kuzungumza lugha ya mama ni dalili ya
ushamba au kinyume chake kwamba kuzungumza lugha ya Kiingereza ni dalili
ya kuwa mtu wa tabaka la juu.
28
Zoezi
Kwa kuzingatia hali ya lugha nchini Kenya, ni kwa njia gani nadharia ya
Umaksi inaeleza hali hii (zingatia mvutano kati ya lugha ya Kiingereza
na lugha nyinginezo za Kiafrika).
Swali
Huku ukitumia nadharia moja ya Elimujamii, onyesha namna lugha
inavyoingiliana na jamii
2.4 HITIMISHO
Katika somo hili tumejadili nadharia mbili za kijamii ambazo zitatusaidia
kuelewa jamii. Nadharia hizi zitachangia katika kuelewa swala la lugha katika
jamii.
Marejeleo Teule
Eagleton, T. (1983) Literary Theory: An Introduction. Oxford: Blackwell.
Mesthrie, R. et al (2001) Introducing Sociolinguistics, Edinberg,Edinberg
Universtity Press.
Wamitila, K.W. (2002) Uhakiki wa fasihi: Misingi na Vipengele vyake. Nairobi.
Phoenix Publishers Ltd.
29
SOMO LA TATU
LUGHA NA JAMII
DHANA ZA KIMSINGI KATIKA ISIMU-JAMII
3.0 Utangulizi
Katika somo hili, tutashughulikia dhana za kimsingi katika isimujamii. Dhana hizi
ni pamoja na lugha, lahaja, mtindo-pekee, sajili au mtindo na jumuiya lugha.
Tutazingatia dhana hizi kwa kuonyesha maana yazo pamoja na kuonyesha jinsi
zinavyohusiana na uwanda mzima wa isimujamii.
3.1 Madhumuni
Baada ya kulipitia somo hili, tunatarajia kwamba utaweza:
1. Kueleza maana ya lugha na matumizi yake.
2. Kueleza maana ya lahaja na jinsi lahaja zinavyoibuka.
3. Kueleza maana ya mtindo-pekee.
4. Kueleza maana ya mtindo na sajili pamoja na kueleza sajili mbalimbali.
5. Kueleza ni nini maana ya jumuiya lugha.
3.2 Lugha
Lugha ni chombo kilichoundwa na wanadamu kwa ajili ya matumizi yao; kwa
hivyo kama wanadamu wasingekuwapo, hapana shaka kusingekuwapo na lugha
pia. Kutokana na huu uhusiano kati ya lugha na binadamu, ni dhahiri kuwa tabia
na mabadiliko ya wanadamu yataiathiri lugha vilevile (Mdee, 1986). Wanaisimu,
katika kuichunguza lugha, wanaichukua kama kitu na kuanza kuifafanua,
wakiangalia miundo ya vipengele mbalimbali vinavyoijenga na kuikamilisha na
jinsi inavyoathiriwa na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na
kisaikolojia ya wazungumzaji.
30
Swali
Je, lugha ni nini?
Kujibu swali hili ni rahisi kwa sababu wanaisimu mbalimbali wamejaribu kutoa
mawazo yao juu ya swali hili. Hebu tuangalie wanachokisema wanaisimu.
Kwa mujibu wa Otto Josepersen, Encyclopedia Britannica, lugha ni njia yoyote ya
mawasiliano kati ya viumbe vyenye uhai. Kwa maana hii lugha ina maana kubwa
sana. Tunaona kwamba fasili hii inaeleza kimantiki kuwa kila kiumbe chenye
uhai kina lugha. Kwa hivyo, tunapata lugha kwa wanadamu, wanyama, wadudu
na mimea.
Kwa maana yake maalum lugha ni njia yoyote wanayoitumia wanadamu katika
kuwasiliana. Maana hii ni sawa kidogo na hiyo ya mwanzo lakini mkazo
umetiliwa kwa wanadamu tu. Maana hii inalingana na Trudgil (1974) katika
Sociolinguistics anayesema kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa
kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake.
Kwa maana ya kiisimu, lugha ni utaratibu wa sauti za kusemwa, za nasibu, za
jamii yenye utamaduni fulani ambazo huzitumia kwa kuwasiliana. Hapa,basi,
tunaona kwamba maana hii inabagua kabisa maana zake tulizotaja mwanzoni.
Kwa kutumia maana hii,hebu tuchambue kila kipengele:
Lugha:
(a) ni sauti ya kusemwa. Mtu hutoa sauti fulani ambayo ina maana.
Tunatumia midomo, taya, ulimi, meno, koo, nyuzi, ufizi na kadhalika.
(b) ni sauti za nasibu. Sauti hizi zimetokea tu kwa bahati katika ile lugha
isemwayo. Hakuna kitu kilichofanyika kupatana juu ya maneno. Kwa
31
mfano, maneno haya haya ya lugha mbalimbali huwakilisha neno kiti
endeve (kimaragoli), chair (Kiingereza) na kadhalika.
(c) ni sauti zenye utaratibu kamili. Sauti za lugha yoyote huwa zimepangwa
kwa kufuata utaratibu fulani unaokubaliwa na jumuia hiyo ya watu.
Utaratibu huo huitwa sarufi. Kwa mfano, hatusemi Maria tunda ana bali
jumuia imepatana kusema Maria ana tunda .
(d) ni sauti ya watu wa utamaduni fulani. Utamaduni ni mila na desturi za
maisha ya watu zilizojengwa tangu awali. Lugha inatawaliwa na maneno
ya utamaduni wa watu hao. Kwa mfano, wazungu wana maneno mengi
ya sayansi wakati Waafrika hawana maneno ya kuelezea, k.m. motokaa,
santuri na kadhalika ni vitu ambavyo havikuwapo katika utamaduni wao.
(e) ni sauti za kueleza wazo. Yaani ni sauti zinazowawezesha watu kupashana
au kujulishana habari.
3.2.1 Matumizi ya Lugha
Kwa jumla matumizi ya lugha yoyote hutegemea:
(a) Mahali, kwa mfano nazi kwa watu wa pwani.
(b) Wakati, kwa mfano, maneno ya kisiasa ya miaka hii kama vile, uwazi, haki
za binadamu na kahdalika.
(c) Umri, kwa mfano, maneno ya sheng ambayo hutumiwa zaidi na vijana.
(d) Hali ya kike au ya kiume, Kwa mfano, Aka kwa mwanamke, Ebo kwa
wanaume, Bee kwa wanawake na Naam kwa wanaume.
(e) Kisomo, kwa mfano, ziara badala ya safari, stashahada badala ya cheti
na kadhalika.
(f) Pia matumizi na mabadiliko ya lugha yanaweza kutegemea jadi, ada, kazi
au daraja ya mtu.
32
Swali
Jadili kauli kwamba Lugha na jamii hukamilishana na kuathiriana
3.2.2. MITAZAMO ELEZI NA ELEKEZI YA LUGHA
(i) Mtazamo elezi wa lugha ni ule ambao unafafanua vipengele vya lugha
jinsi vilivyo. Ni mtazamo unaochunguza na kuweka wazi jinsi makundi tofauti ya
watu yanavyoitumia lugha katika miktadha mbalimbali. Uchunguzi kama huu
haupendelei lugha ya kikundi kimoja kuwa ni bora kuliko ile ya vikundi vingine.
Kwa mfano, mtu anaweza kuelezea lugha inayotumiwa darasani, ya wafanyakazi
wa viwanda, ya wachuuzi mjini Nairobi, n.k, bila ubaguzi wo wote.
(ii) Mtazamo elekezi wa lugha huhusika na kanuni au adabu katika lugha.
Huu ni mtazamo ambao unajaribu kuweka sheria za matumizi sahihi ya lugha ili
watumiaji wa lugha walazimike kuzifuata sheria hizo.
Mtazamo elekezi hujitokeza vizuri zaidi katika sarufi mapokeo, ambapo dhima ya
mwalimu wa lugha inaonekana ni kuhakikisha kuwa lugha safi au nzuri
inahifadhiwa na kutumiwa. Hapa kanuni zinatolewa kuhusu vipashio mbalimbali
vya matumizi ya lugha kwa mfano:
Sarufi: Sentensi huanza kwa herufi kubwa.
Msamiati: Msamiati unaofaa umetumika.
Maana: Kwamba mtu amemaanisha kile alichonuia.
Matamshi: Mtu ametamka sauti ipasavyo.
Wanaoshikilia mtazamo huu wamejitetea kwa hoja zifuatazo:
1. Kuna matumizi ya lugha yaliyo bora na yenye mantiki kuliko mengine.
2. Wanarejelea mifumo iliyothibitika kuwa mizuri (classical form). Wakati
mwingine wanasarufi hutilia mkazo uamuzi wao kwa kurejelea lugha
33
zilizodhaniwa kuwa bora hapo zamani. Lugha kama Kilatini, Sanskrit,
Tamil na Kiarabu zilichukuliwa kuwa vielelezo vya kuigwa. Mara nyingi
Kiingereza kililazimishwa kufuata mfumo wa Kilatini ili kionekane pia kuwa
sahihi.
3. Hupendelea mifumo ya zamani ya lugha hiyo.
Wanaoshikilia mtazomo elekezi katika lugha huwa hawataki kuiona lugha
yao ikipitia mabadiliko yo yote. Hawataki visawe viongezeke, au maana,
au mabadiliko ya kimuundo, yajitokeza katika lugha.
4. Wanakataza matumizi ya maneno ya kigeni.
Huwa hawataki kukopa maneno ya kigeni na kuyatumia katika lugha zao.
Kwa mfano, huko Ufaransa kuna taasisi inayoitwa The French Academy
(Chuo cha Ufaransa) ambayo ina kazi ya kukitakasa Kifaransa kwa
kuondoa maneno yote ya lugha nyingine, hasa Kiingereza,
yanayojipenyeza kwenye lugha hiyo.
Wanaopinga mtazamo elekezi wa lugha wanasisitiza kwamba lugha zote ni sawa,
hakuna lugha au lahaja iliyo bora kuliko nyingine. Wanaisimu wanasema kuwa
misingi ya lugha elekezi imejikita katika matumizi ya lugha au kiisimu ya watu
wa tabaka la juu katika jamii, na si katika dhana ya usawa. Wamesema
yafuatayo katika kuupinga mtazamo huo:
1. Mtazamo wa kimantiki wa lugha kama vile ilivyo katika hisabati una
matatizo. Kama utafiti wa sarufi uliofanywa na Chomsky (1965)
ulivyoonyesha, kutatokea utata mwingi kwani sheria za lugha ni chungu
nzima.
2. Wanasema kuwa kila lugha ina upekee wa aina fulani. Kwa hivyo, hakuna
haja ya kulazimisha lugha fulani kufuata mfumo wa lugha kielelezo au
iliyochukuliwa kuwa bora hapo zamani.
3. Kuhusu matumizi ya mifumo ya zamani ya lugha, wanaisimu wanasema
kuwa daima lugha, hubadilika kwa njia mbalimbali. Sheria mpya
34
zinapoibuka zinaingiliana na zile za zamani. Hili haliathiri ubora wa lugha
hiyo.
4. Wanaisimu elezi wanasema kuwa lugha zote hukopa maneno. Ukopaji wa
maneno ni sehemu muhimu ya ukuaji wa lugha. Mara nyingi mabadiliko
yanayotokea katika lugha huakisi mabadiliko yanayotokea katika jamii
kama vile vitu vipya, mitindo mipya, nk.
3.2.3 MJADALA ZAIDI
Kwa muda mrefu wanaisimu wamepuuza mtazamo elekezi katika kuifafanua
lugha. Hata hivyo, inafikiriwa kwamba ikiwa kusudi ni kuzungumzia matumizi
yote ya lugha na mielekeo kuhusu lugha basi, wanaisimu jamii sharti watambue
mtazamo elekezi. Matumizi mabaya na mazuri ya lugha yapo katika jamii.
Kama vile usafi ulivyo muhimu kwa afya bora, ndivyo lugha sahihi inavyohitajika
katika matumizi ya kila siku ya lugha.
Pili, hata wale ambao wanaupinga mtazamo elekezi huwa wanatumia lugha
sahihi katika maandishi na matamshi yao. Wakati mwingine wahakiki hukosoa
wanaisimujamii kwa kuhimiza au kukubali lahaja zote huku wao wanatumia
lahaja au lugha sanifu. Hata darasani watawaadhibu wanafunzi wao kwa
kutotumia lugha sanifu. Kwa hivyo, hatuwezi kuepuka kuwepo kwa kanuni za
lugha.
Inaonekana basi kwamba mtazamo wa kati unahitajika; ule unaozingatia pande
zote mbili. Katika matumizi yasiyo rasmi tunaweza kuitumia lugha tunavyotaka
lakini katika miktadha rasmi, kama ufundishaji wa lugha darasani, tutumie lugha
sanifu.
Hata wanaisimujamii hualikwa kama wataaalamu kushiriki katika upangaji wa
lugha. Katika hali kama hizo, wao huulizwa kufanya uchaguzi kuhusu vibadala
fulani vya lugha vinavyofaa, maneno na misemo. Hivyo basi wanaisimujamii
35
hawawezi kupuuza wazo kwamba ubora wa lugha ni sehemu ya mazingira ya
lugha katika jamii nyingi.
Zoezi
Huku ukitumia mtazamo elekezi, toa mifano kumi ya makosa yanayofanywa
na watu katika lugha kisha urekebishe makosa hayo.
3.3 LAHAJA
Imethibitika kuwa lugha haitulii, huenda ikibadilika kila wakati. Hata katika
lugha ya kundi moja, tofauti nyingi hudhihirika. Crystal (1995:3) amezungumzia
vibadala vifuatavyo vya lugha.
Vibadala kijamii/kitabaka
Vibadala vya muda
Vibadala kibinafsi Vibadala kimaeneo
Jinsi lugha inavyotofautiana kimfumo ni jambo linalowashughulisha
wanaisimujamii. Lugha pia inaweza kubadilika kulingana na muktadha, wakati
na mzungumzaji au mhusika. Katika somo la isimujamii msisitizo huwa ni kwa
kikundi cha jamii na wala sio kwa mtu binafsi. Taaluma ya lugha
inayoshughulikia lahaja kwa ujumla huitwa elimulahaja (Dialectology).
3.3.1 MAANA YA LAHAJA
36
Lahaja ni mojawapo ya migao ya lugha ambayo hutokana na mabadiliko ya
lugha. Chambers & Trudgill (1980:3) wanaeleza kuwa katika matumizi ya kila
siku, ambayo yana upotoshi fulani, lahaja ni lugha ya kiwango cha chini ambayo
haijakua vizuri, isiyo fahari, na inayohusishwa na makabwela. Katika matumizi
kama haya, inachukuliwa kwamba lahaja huzungumzwa katika sehemu za dunia
zilizojitenga na ni aina ya uzungumzi ulio na mushkili na usiofuata kanuni za
lugha sanifu. Lakini tunajua kwamba mawazo haya hayana msingi wo wote.
Katika lugha tunaamini kwamba hakuna lugha au lahaja iliyo bora kuliko
nyingine duniani lugha au lahja zote ni sawa.
Tunaweza kusema kuwa lahaja ni aina ya uzungumzaji unaotumiwa na kikundi
cha watu aghalabu katika eneo maalum, na hutofautiana na uzungumzaji wa
vikundi vingine vya lugha hiyo moja katika matamshi, msamiati na kwa nadra
sana sarufi.
Inaonekana kuwa lahaja ni kama matagaa ya lugha moja. Mkusanyiko wa lahaja
huunda lugha. Aina hizi za uzungumzaji hazitatizi mawasiliano kati ya vikundi
mbalimbali vya jamii vinavyozungumza lugha moja. Inaonekana kuwa kila mtu
huzungumza lahaja.
Lahaja sanifu huwa na hadhi ya juu kuliko zile lahaja zingine kwani huwa
imeendelezwa kimsamiati na kimuundo.
3.3.2 KUZUK KWA LAHAJA
Kuzuka kwa lahaja mbalimbali duniani ni dhihirisho kuwa daima lugha
inabadilika. Wakati mwingine haya mabadiliko hukithiri kiasi kwamba hakuna
uelewano. Inapotokea hivyo, basi zile lahaja hujitosheleza zenyewe na kuwa
lugha kamili. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Kilatini ambapo lahaja kadhaa
37
zilibadilika na kuwa lugha za Kifaransa, Kihispania, Kiitaliano, Kireno, na
Kiromenia (Wardhaugh 1987).
Kuna mambo matatu muhimu katika uzukaji wa lahaja. Mambo hayo ni:
(a) vizuizi
(b) umbali
(c) muda
(i) Vizuizi (Barriers)
Lahaja huzuka kutokana na vizuizi vinavyoibuka kati ya makundi ya watu
wanaozungumza lugha moja. Vizuizi hivi vinaweza kuwa vya kijiografia kama
vile bahari, mito, milima, misitu mikubwa, n.k. Vizuizi vinaweza pia kuwa vya
kisiasa kama vile mipaka, uongozi, n.k. Vinaweza pia kuwa vya kijamii kama vile
rangi ya mtu, kabila, tabaka, dini, n.k; au vinaweza kuwa vya kiuchumi.
(ii) Umbali (Distance) na Muda (Time)
Watu wanaozungumza lugha moja wakihamia maeneo tofauti na kutengwa na
wenzao kwa umbali fulani, baada ya muda lugha yao itaanza kuwa tofauti
hasa ikiwa hakuna uhusiano mkubwa wa kimawasiliano kati ya makundi hayo.
Pia tunajua kwamba lugha hupokezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, na
baada ya muda mabadiliko ya kimatamshi na kisarufi yanayoletwa na kizazi
kipya hukita. Mabadiliko haya yakikosa kusambaa katika eneo lote basi tofauti
zinajitokeza na tofauti hizi ndizo zinazoitwa lahaja.
3.3.3 NADHARIA YA MAWIMBI (WAVE THEORY)
Nadharia ya mawimbi inaweza kutumiwa kuonyesha jinsi lahaja huibuka.
Mwasisi wa nadharia hii ni Johanness Schmidt (1872). Inasemekana kuwa
mabadiliko ya kiisimu husambaa nje kuanzia kwenye kitovu fulani vile ambavyo
mawimbi yanafanya unapotupa jiwe kwenye kidimbwi. Mawimbi haya
38
yanatofautiana kwa ukubwa na yatakuwa na vitovu tofauti. Jinsi mawimbi
yanavyosafiri kwenda mbali yanazidi kufifia.
Mawimbi haya ya mabadiliko husafiri kupitia kwa maeneo ya kijiografia au ya
kijamii au yote mawili. Yanaweza kuzuiwa au kupunguziwa kasi na vizuizi kama
tabaka, jinsia, umri, kijiografia, n.k. Mabadiliko haya huwasilishwa na watu
binafsi, na wakati fulani badiliko litakuwa limefikia watu fulani na kutowafikia
wengine.
3.3.4 ISTILAHI ZINAZOTUMIKA KATIKA LAHAJA
(i) Kizingasifa (Isogloss)
Katika utafiti wa lahaja tunaweza kuchora ramani kuonyesha mahali ambapo
matamshi, msamiati au muundo fulani hutumiwa. Kuna njia mbili za kuonyesha
mambo haya:
(a) Kwa kutumia ishara
(b) Kwa kuunganisha sehemu hizo kwa laini inayoitwa kizingasifa.
Kizingasifa ni mpaka unaochorwa kulizungushia eneo ambalo lina sifa maalum za
matamshi, sarufi au msamiati katika ramani ya kiisimu.
Kizingasifa hutumika ili kutenganisha sehemu zilizo na sifa fulani na zile ambazo
hazina sifa hizo. Tazama mchoro huu.
Kizingasifa
39
Ruwaza ya vizingasifa huelezwa kwa kuzingatia vizuizi vya kijiografia ambavyo
vinatenganisha jamii mbili au zaidi zilizopakana. Vizuizi hivi ni kama mto wenye
kina kirefu, msururu wa milima, n.k. Vizuizi vinaweza kuwa ni vya kijamii au
kisiasa. Watu wa eneo fulani wanaweza kuwa na mfumo tofauti wa kisiasa na
kijamii na hivyo wakawa na utamaduni tofauti na maeneo waliyopakana nayo.
(ii) Eneo la Fahari (Centre of Prestige)
Vizingasifa vingine huwa na ruwaza inayoonyesha kusambaa kwa kipashio cha
kiisimu kutoka kwa eneo la fahari au kitovu, ambalo aghalabu huwa mji. Hapa,
vizingasifa hivi hufanana na viwimbi vinavyotokana na jiwe lililotupwa majini.
Ndivyo tulivyopata nadharia ya mawimbi. Wanaoshikilia nadharia hii huamini
kwamba mabadiliko ya kiisimu husambaa kama mawimbi.
(iii) Sehemu masalio (Relic Areas)
Wakati mwingine ruwaza hujitokeza ikionyesha sehemu ndogo ndogo ambazo
zimeachana lakini zenye sehemu zinazofanana kiisimu. Sehemu hizi hazina eneo
la fahari kama miji. Hizi ni zile sehemu ambazo hazijafikiwa na miundo mipya.
Mara nyingi sehemu hizi huwa katika maeneo yaliyojitenga kama milima,
mabonde au mipaka ya lugha fulani.
(iii) Sehemu za Mpito (Transitional Areas)
Hii ni sehemu ambayo mawimbi ya eneo la fahari moja hukutana na mawimbi ya
eneo la fahari jingine. Katika hali kama hii eneo hilo halina sifa maalumu
tambulishi bali linashiriki sifa za maeneo mawili ya fahari yaliyo jirani. Kwa
mfano, Luanda, iliyo kati ya mkoa wa Nyanza na Magharibi.
3.5 AINA ZA LAHAJA
Kuna aina mbili za lahaja:
3.5.1. Lahaja za Kijiografia
Hizi ni lahaja zinazozungumzwa katika maeneo fulani, nazo hutokea watu wa
lugha moja wakihamia maeneo tofauti halafu wakatengwa kimawasiliano kwa
40
umbali, milima, bahari, mipaka, n.k (Fromkin & Rodman 1974:254). Mifano ya
lahaja za kijiografia ni zile za Kiswahili: Kiunguja, Kimvita, Kiamu, Kimrima,
Kimgao, Kitumbatu, n.k.
Watu wanaofanyiwa utafiti ili kuthibitisha kuwepo kwa lahaja hizi ni wazee walio
na umri mkubwa ambao wameishi mahali hapo kwa muda mrefu, wana kisomo
kidogo au hawana, na ambao hawajapata athari ya lugha au lahaja nyingine.
Zoezi
Taja lugha nyinginezo mbili unazozifahamu na uonyeshe lahaja zake.
3.5.2. Lahaja za Kijamii/Kitabaka
Hizi ni lahaja zinazotumiwa na makundi ya watu kulingana na hadhi yao, tabaka,
elimu, kazi wanayofanya, pato, umri, uana, na vipengele vingine vya kijamii.
Watu wanaokuwa katika lahaja moja ya kijamii si lazima wawe wanaishi katika
eneo moja.
William Labov, mwanaisimu wa Kimarekani, aliona kuwa lugha inao mfumo wa
vibadala ambao unaweza kuelezwa kuzingatia tofauti za kimatabaka katika jamii
fulani.
Utafiti uliofanywa na watafiti wengi wakiwemo Labov na John Fischer
unaonyesha kuwa watu hutumia vipashio fulani vya kiisimu si kwa sababu ni
rahisi kuvitamka bali kwa sababu ya jinsi wanavyohisi kuhusu hadhi yao na wale
wanaowazungumzia. Kwa mfano kusema:
Maalim badala ya mwalimu
Nchini Kenya, kumekuwepo na lahaja za kijamii kama Kisetla na Kihindi.
41
Zoezi
Je, kuna lahaja zingine zipi za kimatabaka nchini Kenya?
3.6 LUGHA AU LAHAJA?
Vipengele vifuatavyo hutuwezesha kuamua kama tofauti za kiisimu zinazotokea
zinaashiria tofauti za lahaja au za lugha. Unajuaje kuwa jinsi mbili za
kuzungumza ni lahaja za lugha moja au ni lugha mbili tofauti?
3.6.1. Kusikilizana (Mutual Intelligibility)
Ingawa lahaja hutofautiana, watu wanapozungumza huelewana. Ikiwa
wazungumzaji wawili walio na tofauti fulani katika lugha zao wataelewana
wanapozungumza, basi itachukuliwa kwamba wanatumia lahaja tofauti za lugha
moja. Lakini ikiwa hawataelewana basi wanazungumza lugha tofauti. Hata
hivyo, kuna viwango mbalimbali vya kuelewana kati ya lahaja mbalimbali.
Wazungumzaji wa Kinyala na Kibukusu kwa mfano ,wataelewana kwa sababu
hizi ni lahaja za lugha moja, lakini wazungumzaji wa Kiingereza na Kikamba
hawataelewana.Watu wengi husema kuwa kipengele muhimu cha kuamua kama
ni lugha au lahaja ni hiki.
3.6.2. Mwendeleo lahaja (dialect continuum)
Dhana hii hurejelea mfuatano wa jinsi lugha zinavyopakana kijiografia, yaani A
B C D E F G ... Katika mkururo huo, huwa kuna kusikilizana katika
lahaja zilizopakana, lakini zile zilizotengana kwa mbali huwa hakuna masikilizano.
Kwa mfano, kuna uwezekanao kuwa wazungumzaji wa A na G hawataelewana.
Hapa ndipo tatizo linazuka. Je, bado tunaweza kusema kuwa A na G ni lahaja za
lugha moja?
3.6.3. Lugha sanifu
42
Kuwepo kwa lugha sanifu au maandishi yanayotumiwa na kundi la watu
hutusaidia kujua kama zinazohusika ni lahaja au lugha. Ikiwa makundi mawili au
zaidi yanayotofautiana katika maongezi hukubaliana kuwa yana mfumo mmoja
ulio sanifu au yanatumia aina moja ya maandishi, basi inachukuliwa kuwa
yanazungumza lahaja tofauti na wala si lugha tofauti.
Kwa mfano, nchini Uchina wazungumzaji katika sehemu mbalimbali za nchi
hutumia Mandarin, Cantonese, Wu, Hakka au Fukien. Wazungumzaji wa
vibadala hivi hawaelewani lakini kwa sababu wanatumia mfumo mmoja wa
kuandika (wa Kichina) na kusoma basi inachukuliwa kuwa hizo ni lahaja
mbalimbali za Kichina.
3.6.4. Vipashio visivyo vya Kiisimu
Sifa fulani zisizo za kiisimu hutumiwa pia kuamua kama kinachohusika ni lahaja
au lugha. Sifa hizi ni kama utamaduni mmoja, utii wa kisiasa au dhamiri za
wazungumzaji (conscious of the speakers).
Kwa mfano, wazungumzaji wa Cantonese (China kusini ) na Mandarin ( China
Kaskazini) hawaelewani wanapozungumza lakini inachukuliwa kuwa wanatumia
lahaja tofauti za Kichina kwa sababu wote wanaishi Uchina (siasa) na wanashiriki
utamaduni mmoja wa Kichina. Pia wanatumia mfumo mmoja wa maandishi.
Aidha, wazungumzaji wa Swedish, Danish na Norwegian wanasikilizana
wanapozungumza lakini kwa sababu wanaishi katika nchi tofauti na wana
tamaduni tofauti inachukuliwa kwamba wanazungumza lugha tofauti.
Hata pale ambapo sifa za kisiasa hazijitokezi sana, utamaduni pekee hupelekea
wazungumzaji kufikiriwa kuwa wanazungumza lugha tofauti, kwa mfano, Wazulu
na Waxhosa huelewana wanapozungumza, lakini wanahisi kwamba wao ni
tofauti na hata wana lugha tofauti kwa sababu wana tamaduni tofauti. Mfano
43
mwingine ni wa Wasuba na Waluo ambao wanaona kuwa wanazungumza lugha
tofauti.
Swali
1. Je, lugha yako ina lahaja ngapi? Andika maneno yanayotofautisha
lahaja moja na nyingi.
2. Kwa kurejelea nchi ya Kenya ,onyesha zile lahaja ambazo zinaonekana
kuwa
Lugha tofauti ilhali wazungmaji wanaelewana.
3.7 MTINDO-PEKEE
Wazungumzaji wote wa lugha fulani huelewana wanapozungumza, lakini hakuna
watu wawili wanaozungumza kwa namna moja. Tofauti zinazotokea
husababishwa na umri, uana, afya ya mtu, ukubwa, hulka, hali ya kimawazo,
tajriba na ubinafsi wa mtu. Tofauti hizi hujitokeza katika msamiati, matamshi na
kwa kiasi kidogo katika sarufi. Sifa ya namna ya uzungumzi unaohusishwa na
mtu binafsi huitwa mtindo pekee.
Mtindo pekee ni matamshi ya kipekee ya msemaji au mzungumzaji yanayotokana
na athari za mazingira. Hii ina maana kwamba kuna mfumo fulani wa kiisimu
unaohusishwa na kila mzungumzaji. Jambo hili linadhihirika wazi pale ambapo
tunamtambua mtu kupitia kwa matamshi au sauti yake bila kumwona. Kila
mzunguzaji wa lugha ana mtindo wa kipekee wa lugha. Mtindo pekee wa mtu
huweza kubadilika katika vipindi mbalimbali vya maisha yake.
Zoezi
Pambanua tofauti za kiisimu zinazojitokeza miongoni mwa marafiki zako.
44
3.8 MTINDO
Dhana ya mtindo ni tatanishi kwa sababu kuna misimamo na mitazamo chungu
nzima inayotokana nayo. Kwa mfano, dhana ya lafudhi inayomaanisha ubinafsi
katika matumizi ya lugha, inayomtambulisha mtu kama mtu, yaelekea
kupendekeza kuwa labda kuna mitindo mingi ya matumizi ya lugha kama kulivyo
na watumizi wengi wa lugha husika. Kwa hivyo yaonekana kwamba kila mtu
ulimwenguni ana mtindo wake.
3.8.1 Maana ya mtindo.
Ili kutoa maana ya dhana ya mtindo hebu tuangalie yale wanayosema Crystal na
Davy (1969) katika Investigating English Style .Wamefafanua mtindo kwa
kutumia mitazamo ifuatayo.
(i) Mtindo kama tabia za mtu katika matumizi ya lugha.
(ii) Mtindo kama tabia za kimakundi katika matumizi ya lugha.
(iii) Mtindo kama tabia za kitathmini yaani kiupimaji.
(iv) Mtindo kulingana na lugha ya fasihi.
Hebu basi tutoe maelezo ya kila moja.
(i) Mtindo kama tabia ya mtu.
Kwa mujibu wa mtazamo huu, uchambuzi humulika na kuangalia tabia za kiisimu
zinazoambatana na lugha ya mtu katika uyakinifu wake. Neno tabia katika
muktadha huu linatumiwa kumaanisha kanuni za kiisimu zinazotambulisha lugha
ya mtu anayehusika.
Mtindo hutumiwa hapa kurejelea namna mtu anavyotumia lugha. Jambo ambalo
lina upekee fulani wa kiisimu. Huu upekee ndio unaotambulisha na kumsawiri
yeye kama yeye.
Mtazamo huu ndio unaowaruhusu wachambuzi kuzungumza kuhusu mtindo wa
waandishi au wasemaji mbalimbali (tazama Kitsao 1975). Kwa mfano, unaweza
45
kuzungumza kuhusu mtindo wa uandishi wa Shaaban Robert, Ebrahim Hussein
au Said Ahmed Mohamed.
Buffun katika hotuba aliyoitoa mnamo Agosti 27, 1753, alisema kuwa mtindo ni
mtu mwenyewe , na huu umekuwa msingi wa mtazamo huu. Maoni haya
yanajadili kuwa kila mwandishi au msemaji ana lugha yake ambayo hudhihirika
katika kazi zake zote na ambayo humtofautisha na waandishi au wasemaji
wengine. Hivi ni kusema kwamba hulka ya mwandishi inatarajiwa kuonekana au
kudhihirika kutokana na matumizi yake ya lugha.
Uchunguzi unaonyesha kuwa katika kujifunza lugha, kwa kawaida, watu hukuza
na kupalilia tabia fulani za kipekee katika matumizi yao ya lugha. Matokeo ni
tabia za kibinafsi ambazo hubainika kwenye mawasiliano yake. Hivyo basi,
mtindo unakuwa matokeo ya moja kwa moja ya jinsi mtu anavyojieleza
kulingana na tajriba yake katika kujifunza lugha.
Zoezi
Pambanua tabia za kiisimu ambazo zinaibuka katika usemi wa rafiki
yako. Taja elementi tano za kiisimu kwa kila moja ambazo humtofautisha
na mtu mwingine.
Kwa vile imetambuliwa kwamba kuna mitindo mingi kama kulivyo na waandishi
na wasemaji, uchambuzi wa mtindo hauna budi kumshughulikia kila mtunzi
kivyake. Kwa mfano, tunaweza kusema kuwa mwandishi Shabaan Robert
anajulikana kwa matumizi ya sentensi ndefu hata zinazofikia maneno thelathini.
Aidha anatumia uhuishi na jazanda katika kazi zake.
46
(ii) Mtindo kama tabia za kimakundi.
Katika upana wake dhana ya mtindo inaweza kurejelea tabia za kundi la watu
katika matumizi yao ya lugha. Mtazamo huu ndio mhimili wa misingi ya sajili
katika matumizi ya lugha. Kwa hivyo, mtindo wa matumizi ya lugha
unapokubalika kimakundi unakuwa utaratibu unaofaa kuzingatiwa katika sajili
inayohusika.
Kwa mfano, kuna kanuni za kuanzisha na kuhitimisha ngano katika jamii za
Kiafrika:
Msimulizi: Paukwa
Hadhira: Pakawa
Msimulizi: Kaondokea chanjagaa
Kajenga nyumba kakaa
Mwanangu mwana Siti
Kijino kama Chikichi
Cha Kujenga kikuta na
vilango vya kupitia.
Au:
Msimulizi: Hadithi! Hadithi!
Hadhira: Hadithi njoo
Msimulizi: Hapo zamani za kale paliondokea ...
Pia kuna mtindo wa kuandika mashairi ya kimapokeo. Mwandishi anazingatia
idadi ya mizani katika mshororo, vina, idadi ya mishororo katika ubeti na
utoshelezi. Katika uandishi wa tenzi mwandishi huanza kwa ombi na kadhalika.
47
Zoezi
Eleza mtindo unaodhihirika katika bara rasmi na fomu za serikali.
(iii) Mtindo Kiutathmini.
Madhumuni ya kuwasiliana huwekewa vikwazo au mipaka na mtazamo huu
hupima na kutoa masharti kuhusu namna ya kuwasilisha wasilisho fulani.
Mtazamo huu unaongozwa na maoni kwamba kila mtindo unao maneno yafaayo
na mahali pafaapo kwenye muundo wa sentensi. La muhimu hapa ni kwamba,
ujumbe utolewe kwa njia ifaayo kabisa kisarufi na kimaana: Hebu tueleze kwa
kutoa mifano ya sentensi hizi:
1 (a) Kwa sababu ya kuchelea kuwa huenda ng ombe wake akapotea tena,
mchungaji alimkamata na kumfunga miguu ya mbele na ya nyuma kwa
kamba.
1 (b) Kwa sababu ya kuchelea kuwa huenda ng ombe wake akapotea tena,
mchungaji alimkamata na kumfunga kwa kamba miguu yake ya mbele na
ya nyuma.
Katika sentensi hizi mbili tunaona kuwa mpangilio wa maneno ni tofauti.
Zoezi
Eleza tofauti za kimaana zinazotokea katika mifano ya sentensi hapo juu
48
Wakati mwingine, tatizo huwa kubwa zaidi kiasi cha kuhitaji sio tu maneno
kupangwa upya bali pia kurekebishwa au kubadilishwa kwa viwakifishi.
Wataalamu wamefafanua mtazamo huu kwa kutilia mkazo kwamba mtindo mzuri
hutokana na kuchagua taashira zifaazo kwa wasilisho linalonuiwa kuwasilishwa.
Kwa ufupi, uchambuzi wa mtindo kulingana na mtazamo unaohusika hapa ni
kukadiria namna mwasilishi alivyofaulu katika wasilisho lake, kulingana na uteuzi
kimsamiati na kisarufi.
(iv) Mtindo kulingan na lugha ya Fasihi.
Kwa mujibu wa mtazamo huu mtindo ni utunzi wa fasihi ya hali ya juu kabisa.
Hata hivyo tunaona kuwa maelezo haya yanatatiza kimaana kwa sababu
hayazingatii kikamilifu mahusiko ya dhana ya mtindo yenyewe. Vile vile, maoni
haya yanalifinya swala hili la mtindo. Inaonekana kuwa maoni haya yanalenga
umbuji au ubunifu wa kurejelea mbinu za kujieleza kama vile matumizi ya
tamathali za usemi. Lakini mtindo, tunajua ni zaidi ya mbinu hizi. Mtindo sio tu
jinsi waandishi wanavyoandika lakini pia ni njia mbalimbali zinazotumiwa na watu
kuongea au kuandika katika hali za kawaida za kila siku. Kwa hivyo, mtindo ni
jumla ya namna lugha inavyotumiwa na wanajamii.
Swali
Onyesha tofauti zilizopo kati ya:
1. Mtindo kama tabia za mtu na mtindo kama tabia za kimakundi.
49
3.9 SAJILI
Kulingana na Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990) sajili, ambayo pia
inajulikana kama rejista ni lugha inayotumika katika muktadha maalumu. Sajili
huelekea katika kupambanua lugha ifaayo katika miktadha fulani. Sajili
hutofautiana kutegemea mambo kama vile, miundo ya lugha, msamiati, uundaji
wa sentensi, kupanda na kushuka kwa sauti na unyambuaji.
Sajili ni sehemu ya umilisi wa mawasiliano ambao kila mzungumzaji huwa nao.
Umilisi huu humwezesha kubadili matumizi ya lugha, kuteua vipengele fulani vya
matamshi, msamiati na kadhalika katika miktadha mbalimbali.
Akishughulikia swala la sajili, Halliday (1964) alisema kuwa sajili hutofautiana
kutokana na :
(a) Mada inayozungumzwa.
(b) Uhusiano kati ya watu wanaowasiliana. Kwa mfano, nani anashiriki
katika mazungumzo? Ni mtu na mkubwa wake, au ni mtoto na mzazi au
ni rafiki tu?
(c) Njia ya mawasiliano ambayo inatumiwa ikiwa ni andishi au zungumzi au
ishara?
3.9.1 CHANZO CHA SAJILI.
Inawezekana kwamba matumizi ya sajili mbalimbali yameibuka kutokana na
mikatale ya kijamii. Watu wana miiko mbalimbali inayohusu matumizi ya lugha,
kwa mfano, ukitumia lugha inayoambatana na mazingira kama vile inayoonyesha
furaha mazikoni basi huenda ukaathiriwa. Kwa hivyo, lugha imegawika katika
sajili mbalimbali kutokana na imani za watu na pia kukidhi mahitaji ya muktadha.
Mfano mwingine ni kwamba baadhi ya jamii huamini kwamba lazima ngano
zihadithiwe mahali maalumu, wakati maalum na sharti ziambatane na matumizi
maalumu ya lugha.
50
Pili, tunaweza kutuhumu kuwa sajili inatokana na kugawika kwa jamii katika
makundi ya kazi mbalimbali ili kujikimu. Kila kundi likiwa na msamiati
unaoelezea hali, mazingira na zana zake za kazi.
Msamiati huu, na upekee wa uzungumzaji ulizua sajili mbalimbali. Tunaweza
kuhusisha jambo hili na ukuaji wa binadamu kimaendeleo. Jinsi binadamu
alivyoendelea ndivyo kazi mbalimbali zilivyojitokeza na hivyo kukawa na lugha
maalum ya kuelezea hali hizo. Kwa mfano, maendeleo upande wa sayansi na
teknolojia yamezua sajili ya kisayansi na kiteknolojia.
3.9.2 MIFANO YA SAJILI NA SIFA ZAKE ZA KIISIMU
1. Matangazo ya biashara:
Sifa zake
1. Lugha ya mvuto.
2. Lugha ya kimajazi.
3. Lugha shawishi au msukumo (kutaka mtu awe mteja wao).
4. Misemo maalumu inayonasa.
5. Wingi wa porojo.
6. Kuchanganya lugha.
7. Uradidi wa sauti au maneno.
2. Matangazo ya mpira
1. Lugha changamfu 7. Matumizi ya kidato cha juu
2. Lugha ya kutia chumvi. 8. Maswali ya balagha.
3. Lugha batebate. 9. Mbinu rejeshi.
4. Lugha hugeuka kuwa kelele. 10. Msisitizo.
5. Kuchanganya lugha. 11. Kutokamilika kwa sentensi.
6. Uundaji wa msamiati.
51
(Kwa ufafanuzi zaidi wa aina a sajili,rejelea mtaala wa AKS 101)
Zoezi
Taja sifa za sajili zifuatazo:
i. Sajili ya kidini.
ii. Sajili ya sheria-(andishi).
3.9.4MASHARTI YA MATUMIZI
Crystal na Davy (1969) pamoja na Kitsao (1988) wameshughulikia masharti ya
matumizi ya lugha. Haya ni mambo yanayomwongoza mzungumzaji au
mwandishi ili kuteua sajili inayofaa katika mawasiliano yake. Crystal na Davy
(ibid) wameyaita mawanda ya matumizi kimuktadha na wamejadili vipengele
vinane.
1. Ubinafsi
2. Lahaja.
3. Wakati.
4. Kazi.
5. Hadhi.
6. Namna ya kuwasilisha.
7. Upekee.
8. Aina ya mazungumzo
Kitsao (1988) kwa upande wake amejadili masharti kama:
1. Mazingira.
2. Uhusiano.
3. Cheo.
4. Hali.
5. Madhumuni.
6. Kichwa cha mazungumzo.
52
7. Lugha azijuazo mtu.
8. Tabaka na malezi.
9. Umri.
Hebu tutoe maelezo kwa masharti anayotoa Kitsao(ibid)
(i) Mazingira
Kulingana na lugha katika mazingira, itaonekana, kwa mfano, kuwa matangani
kutakuwa na matumizi ya lugha ya huzuni, kupeana mkono wa pole na
kuliwazana. Pia mtu akiwa ofisini analazimika kutumia lugha rasmi lakini
akiingia mitaani miongoni mwa watani atazungumza lugha isiyo rasmi.
(ii) Uhusiano
Uhusiano wa watu katika jamii husababisha lugha kutumiwa kwa mtindo fulani
ufaao. Kati ya mzazi na mwanawe kuna miiko inayowataka wawasiliane kwa njia
ya heshima. Mathalani, si kawaida mzazi na mwanawe kutaniana au mwana
kumwita babake kwa jina lake katika jamii za Kiafrika. Lakini watani wa mtu
huwa na uhuru mkubwa katika matumizi ya lugha miongoni mwao.
(iii) Cheo
Cheo ni muhimu katika matumizi ya lugha kwani kuna lugha anayostahili kutumia
Profesa, kuna lugha ya wazee, lugha ya vijana na kadhalika. Ndiposa tunaweza
kusikia lawama kuwa ijapokuwa fulani ana cheo hazungumzi kulingana na cheo
chake.
(iv) Hali
Ni kweli kwamba lugha ya mtu hubadilika au kuathirika kulingana na hali ya mtu
huyo. Mtu anapokuwa mgonjwa hutumia lugha ya kuvuta huruma. Lugha ya
mlevi huwa legevu na ovyo. Mtu anapokasirishwa hutumia lugha kali na ya
kutisha.
53
(v)Madhumuni
Lugha inaweza kutumiwa kulingana na madhumuni au msimamo wa mtu katika
jambo fulani. Inawezekana kuwa madhumuni ni kuvutia au kuteka watu kiakili
ambapo mwongezi atatumia lugha nyenyekevu na ya ushawishi mkubwa. Lugha
yaweza kutumiwa kwa lengo la kuchukiza, kuchekesha, kuamrisha kupiga
vijembe na kadhalika.
(vi) Kichwa cha Mazungumzo
Sajili mbalimbali zitafaa kwa vichwa tofauti vya mijadala. Kwa mfano, ikiwa watu
wanazungumza juu ya mambo ya kisheria itabidi warejelee sajili ya kisheria kwa
kutumia istilahi zifaazo kama hakimu, mshtakiwa, wakili na kadhalika. Katika
mazungumzo kama haya haitakuwa muhali kuingiza sajili ya matangazo ya
mpira. Maoni yetu ni kwamba vichwa mbalimbali vya mada ndio msingi wa sajili.
(vii)Lugha azijuazo Mtu
Sharti hili ndilo msingi wa kubadili msimbo. Mtu asiyejua Kiingereza hataingiza
lugha hiyo kwenye matumizi yake ya lugha. Lakini yule anayefahamu lugha
nyingine anaweza kuzitumia lugha hizo zote kwa pamoja.
(viii) Tabaka na Malezi
Tabaka na malezi tofautitofauti hukuza viwango mbalimbali vya ujuzi wa lugha.
Jinsi mtu anavyowezesha kutalii na kumudu lugha kikamilifu ndivyo
atakavyoweza kuitumia kwa ukwasi na ufasaha zaidi. Mtu mwenye malezi
mazuri huchuja lugha yake lakini mwenye malezi mabaya hutumia lugha yenye
matusi.
(iX) Umri
Inaonekana kuwa lugha miongoni mwa jamii hukua na kukomaa kulingana na
jinsi mtu anavyokua kutoka utotoni hadi uzeeni. Kwa hivyo, mtoto anapotumia
54
lugha isiyokuwa na ustaarabu kama Naenda kukojoa , kijana wa makamo
atatumia lugha yenye heshima kidogo kwa kusema Naenda haja ndogo ilhali
mzee atatumia lugha fiche kama vile Naenda kutema mate .
Bila shaka kunayo masharti mengi sana yanayosimamia matumizi ya lugha lakini
hayo machache yanatosha.
Zoezi
Eleza kwa kutoa mifano, jinsi kila moja ya masharti hayo
yanavyoweza kuathiri lugha anayotumia mtu.
3.10 JUMUIA LUGHA
Kimsingi, wana-elimujamii huchunguza jamii kwa kuzingatia kategoria kama vile
matabaka, ukoo, usehemu na uchumi.
Dhana ya Jumuia ni neno linalorejelea ile hali ya kundi la watu kufahamu jambo
fulani kwa pamoja, au wana umiliki sawa wa tabia zinazofanana. Wanaisimu
huhusisha dhana hii ya Jumuia na swala la lugha, ndipo tunapata dhana ya
Jumuiya lugha.
Kulingana na TUKI (1990) jumuia lugha ni kundi la watu wanaokaa katika eneo
moja na kutumia namna moja ya lugha.
Kimsingi dhana hii inasisitiza kwamba tabia au matendo ya lugha yanaweza kuwa
kitu ambacho kinaunganisha kundi fulani la watu. Hata hivyo, kumekuwepo na
utata mwingi juu ya maana halisi ya dhana hii. Jambo hili linadhihirika wazi
kutokana na jinsi wataalamu mbalimbali walivyoifasiri.
55
Yule (1996) anasema kuwa jumuia lugha ni kikundi cha watu ambao wana kaida,
sheria na matarajio ya pamoja kuhusiana na matumizi ya lugha.
Lyons (1970) anasema kuwa, jumuia lugha ni jumuia ya watu wanaotumia lugha
moja (au lahaja moja).
Kutokana na maelezo haya, jumuia lugha zinaweza kuingiliana (kwa mfano, pale
kuna watu ambao wanaongea lugha zaidi ya moja) na watu hawa hawahitaji
kuwa na umoja wowote wa kijamii au kitamaduni. Ukweli ni kwamba ni rahisi
kutenga jumuia lugha kwa njia hii, kwa sababu tunaweza kuzitenganisha lugha
na lahaja.
Hocket (1968), Bloomfield (1933) na Gumperz (1962) wanakubaliana kuwa kila
lugha huifasiri jumuia lugha na kwamba jumuia lugha ni kundi la watu
wanowasiliana ama moja kwa moja au kwa njia nyingine kupitia kwa lugha moja.
Katika fasiri hii, tunaona kuwa kigezo cha muingiliano wa mara kwa mara
kinajitokeza. Hii inaweza kuchukuliwa kuwa, ikiwa jamii mbili zinazozungumza
lugha moja lakini hazina utagusano basi zitachukuliwa kuwa jumuia lugha tofauti.
Fasiri hii imeondoa msisitizo wa lugha ya pamoja na kuzingatia mawasiliano.
Nao Hymes (1972) na Halliday (1978) wanasema kuwa, tunapozungumzia
jumuia lugha ni muhimu kuzingatia sheria za pamoja za uzungumzaji na ufasiri
wa matendo ya uzungumzaji. Katika fasiri hii, tunaona kuwa msisitizo unawekwa
kwa jumuia lugha kama ni kikundi cha watu ambao wanahisi kuwa wao ni
jumuia.
Naye Labov (1972) anatilia mkazo mielekeo ya watu kwa lugha na thamani zao
kuhusu miundo ya lugha na matumizi.
56
Fasiri hizi zote ni sahihi kwa sababu zinaeleza jumuia lugha ni nini. Kutokana na
fasiri hizi basi tunapata sifa zifuatazo za jumuia lugha:
1) Ni kundi la watu.
2) Watu wanaowasiliana kwa lugha moja.
3) Wanaweza kuwa wanaishi eneo moja au maeneo tofauti.
4) Kuna mtagusano au kuingiliana kwa watu hawa mara kwa mara.
5) Ni watu walio na mielekeo sawa kuhusu lugha.
6) Ni watu walio na utamaduni sawa.
Swali
Je, unaweza kusema kuwa Kenya ni Jumuia-lugha moja? Toa sababu
za kukubali au kupinga taarifa hii.
HITIMISHO
Maswala kadha wa kadha ya lugha yameshughulikiwa katika somo hili.
Tulianza kwa kueleza maana ya lugha pamoja na matumizi yake. Kisha
tuliona kuwa lugha huweza kujitenga katika makundi mbalimbali ambayo
yanajulikana kama lahaja. Tuliona jinsi lahaja inavyozuka, na tukarejelea
nadharia ya mawimbi kutilia msingi hoja hii. Vile vile tuliona jinsi mtu
anavyoweza kutambua lahaja na lugha. Swala la mtindo pekee kama
ishara ya tabia za kiisimu za mtu fulani limejadiliwa. Isitoshe, swala la
mtindo na sajili vimeshughulikiwa kwa kuchunguza jinsi lugha inavyotumiwa
na vikwazo vinavyosimamia matumizi ya lugha. Na mwisho, dhana ya
jumuiya-lugha imeelezwa.
57
Marejeleo Teule
1. Chacha, L.M. na wengine (2003) AKS 100: Introduction to the Study of
Language: Kiswahili Module. Nairobi. Institute of Open Learning,
Kenyatta University.
2. Chambers, J.k. & Trudgill P. (1980) Dialectology. Cambridge. Cambridge
University Press.
3. Crystal, D. and Davy, D. (1969) Investigating English Style. New York:
Longman.
4. Fromkin, V. & Rodman, R. (1988) An Introduction to Language, New York
Harvourt Brace. Jovanivich College Publishers.
5. Halliday, M.A.K. et.al. (1964) The Linguistic Science and Language Teaching.
London. Longman.
6. Kitsao, J. (1975) A Stylistic Approach Adopted for the Study of Kiswahili
Prose Texts . M.A. Thesis: Nairobi University. (haijachapishwa).
7. Lyons, J.L. (ed.) (1970) New Horizons in Linguistics. Penguin Book.
8. Mdee, J.S. (1986) Kiswahili: Muundo na Matumizi Yake. Nairobi,
Intercontinental Publishers Ltd.
9. Musau, P.M. (1990) Swahili Part Three: Kiswahili in the Twentieth Century.
Nairobi: University of Nairobi.
10. Onyango, J.O. (2002) AKS 102: Historical Development of Kiswahili: Kiswahili
Module. Nairobi. Institute of Open Learning, Kenyatta University.
11. Ryanga, S. na Mukobwa, M. (2003) AKS 101: Language Skills in Kiswahili1 :
Kiswahili Module: Nairobi Institute of Open Learning, Kenyatta
University.
12. TUKI (1990) Kamusi Sanifu ya Lugha na Isimu. Dar es Salaam, University
of Dar es Salaam.
13. Wardhaugh, R. (1987) Languages in Competition, Oxford, Basil Blackwell
Co.
58
SOMO LA NNE
LUGHA ZA MAWASILIANO PANA
4.0 UTANGULIZI
Katika somo hili, tutashughulikia lugha za mawasiliano pana. Hizi ni lugha
ambazo zinavuka mipaka ya jamii moja. Tutajadili hizo pamoja na dhana za
lingua franka, Pijini na Kirioli.
4.1 Madhumuni
Baada ya kulipitia somo hili, tunatarajia kwamba utaweza:
1. Kueleza maana ya lingua franka.
2. Kueleza maana ya Pijini na Kirioli na kuonyesha kuibuka kwa lugha hizi.
4. 2 Lingua Franka
Lingua franka ni lugha inayotumiwa kama chombo cha mawasiliano kati ya watu
ambao hawana lugha moja asilia wanayofahamu wote. Hii ni lugha inayotumiwa
na watu wote katika eneo kubwa hata kama wana lugha zao nyingine. Kwa
mfano, Kiingereza ni lingua franka ya ulimwengu wote. Wakati fulani Kifaransa
kilikuwa lingua franka ya itifaki (diplomacy) na kilatini kilikuwa pia lingua franka
ya dini ya Ukristo.
Baadhi ya lugha zinazotumiwa kwa maana hii, kwa mfano, Kiingereza na
Kifaransa si za kiasili bali huwa zimefahamika kupitia kwa elimu ya shuleni au
elimu rasmi. Hata hivyo, lingua franka nyingine barani huwa za kiasilia na
hupata jukumu hilo kutokana na kabila linalohusika kuwa na nguvu za kisiasa
kama vile Luganda; au kwa kuwa wafanyibiashara mashuhuri kama vile Kiswahili.
59
Kihausa ni lingua franka ya Afrika Magharibi kwa sababu ya nafasi yake katika
biashara.
Kiyunani kilikuwa lingua franka hapo zamani hasa kwa sababu ya vita vya
Alexander the Great .
Kilatini vile vile kilikuwa lingua franka katika nchi za magharibi kwa sababu ya
upanuzi wa utawala wa Roma.
Lugha ya Kiswahili inaweza kudai kuwa lingua franka ya sehemu za Afrika
Mashariki na kati. Jambo hili ni wazi hasa tukizingatia lugha mbalimbali ambazo
zinatumika katika sehemu hii. Kando na hayo, Kiswahili bado kimebakia imara
hata katika hali ya ushindani kutoka kwa lugha mbili zilizo na nguvu yaani
Kiingereza na Kifaransa. Kiswahili kimeweza kuendelea sana hata katika
mazingira hatari, hasa kuanzia kipindi cha kwanza cha karne ya 18 na karne
iliyopita. Ni lugha ambayo inatumiwa sana katika sehemu nyingi za Afrika
Mashariki na Kati.
Baadhi ya lingua franka nyingine katika bara la Afrika ni Bambara na Wolof,
ambazo zote zinapatikana Afrika Magharibi, (Chimera 2000).
Swali
Kiswahili sio lugha ya Afrika Mashariki tu, bali ni lugha ya Kimataifa.
Fafanua kauli hii.
4.3 PIJINI NA KIRIOLI
Utafiti katika lugha za kipijini na kikirioli unakisiwa ulianza mnamo mwishoni mwa
karne ya 19 na mwansaisimu-jamii, Hugo Schuchardt, Swale (1997).
60
Yasemekana kuwa alichapisha mfululizo wa vitabu vilivyojulikana kama
Kroelische Studien katika miaka ya 1880.
Hata hivyo, somo hili lilipuuzwa. Lakini baada ya kupuuzwa, utafiti katika
nyanja ya pijini na kirioli ulianz hasa mwanzo mwanzoni mwa karne ya 20.
Kufikia mwaka 1945 ndipo wanaisimu walipojitosa tena katika utafiti wake. Tafiti
chache zilifanywa katika kipindi cha vita vikuu vya kwanza na vya pili. Baadhi ya
wanaisimu wa mwanzo kutafitia pijini na kirioli ni pamoja na Jacobs (1932), Boas
(1933), Reinecke na Tokimasa (1934), Hall (1948, 1953) na Turner (1949).
4.3.1 SIFA BAINIFU ZA PIJINI
Wanaisimu-jamii wengi wameafikiana kuwa, lugha za kipijini na krioli ziliibuka
katika miktadha ya kibiashara na katika zama za biashara ya utumwa. Lugha hizi
ziliibuka ili kuwawezesha watu walioongea lugha tofauti tofauti kuwasiliana kwa
dhamira fulani fulani. Kama asemavyo David Decamp (1975:15),
Pijini ni lugha ya mawasiliano na ambayo kwa hali za kawaida,
si lugha asilia ya watumizi wake.
Pijini nayo, huwa krioli pale inapopata waongeaji wazaliwa, yaani pijini
inapokuwa ni lugha ya kwanza ya mtu. Muhlhauster (1986:1) anasema ya
kwamba, dhana ya pijini huenda ilitokana na hali au miktadha ifuatayo:
(i) Kutokana na matamshi ya jamii ya Wachina ya neno la Kiingereza
business .
(ii) Kutokana na neno la Kiyahudi pidjom .
(iii) Kutokana na neno Pidian la Wahindi wekundu wa Amerika Kusini; na
(iv) Kutokana na matamshi ya jamii ya watu wa Bahari za Kusini ya neno
beach .
Tunaporejelea asili na miktadha mbalimbali hapo juu, inatubainikia wazi kuwa
lugha za kipijini ziliibuka miongoni mwa jamii za watu walioongea lugha
61
tofautitofauti kwa minajili ya kufaulisha mawasiliano baina yao (Tazama Chacha
na wengine katika AKS 100: Introduction to the Study of Language).
Mwanaisimu-jamii Loreto Todd (1990) anapambanua na kutofautisha pijini-finyu
na pijini-pana.
(i) Pijini-finyu
Pijini-finyu huibuka katika muktadha wa dharura sana kati ya jamii za watu
wanaoongea lugha tofauti. Pijini zinazoibuka katika miktadha ya aina hii, huwa
na sifa bainifu zifuatazo:
(a) Huwa na miundo sahili hasa ya kisintaksia na aghalabu, huhusisha kauli
za kuamrisha na huambatisha ishara za kimwili kama za mikono, macho
na viungo vingine vya mwili. Kwa mfano, pijini za Afrika Magharibi
zilizoibuka kipindi cha vita vikuu kati ya askari jeshi Waingereza na
wenyeji wa eneo hilo.
(b) Idadi kubwa ya msamiati hutokana na lugha ya tabaka la juu au tawala,
na kutiwa kwenye mfumo wa matamshi ya lugha ya wenyeji. Todd
anadai kuwa Kisetla kilichotumika nchini Kenya kati ya masetla wazungu
na Waafrika ni mfano mwafaka. Hili ni jambo ambalo wanaisimu
wanaweza kulitafitia ili kulithibitisha.
(c) Aghalabu pijini finyu huhusisha lugha mbili tu na uhusiano kati yazo
unapokatishwa basi pijini ile hufa. Miktadha yake aghalabu huwa ni ya
dharura za kimawasiliano kama vile katika shughuli za biashara, shughuli
za kijeshi na hii leo, katika shughuli za sekta ya utalii.
(ii) Pijini – Pana
Sifa za pijini-pana ni kamai zifuatazo:
(a) Huibuka kutokana na kudumishwa kwa mazingira ya pijini finyu.
62
(b) Maneno ya pijini finyu yanapopanuka huwa ni lugha ambayo bado
haijakuwa thabiti kimuundo, kimsamiati na kadhalika bali ni matumizi yake
yanayopanuka.
(c) Inapoimarika na kupata waongeaji wazaliwa, basi huwa ni kirioli na
hatimaye inaweza ikawa lingua franka (lugha sambazi) ya eneo fulani la
kijiografia.
4.3.2 Dhana ya Kirioli
Bickerton (1971) anasema kuwa, lugha za kikirioli zinaweza kuibuka kutokana na
miktadha au mazingira yafuatayo:
(a) Pijini zilizopata wazungumzaji wazaliwa.
(b) Katika jamii ambamo asilimia ishirini (20%) ya waongeaji ni wenyeji na
asilimia themanini (80%) ni ya matumizi ya lugha zingine za kigeni.
(c) Krioli huwa na miundo iliyoimarika ya kisarufi msamiati mpana na
kadhalika na hazitumii ishara (kwa wingi) wala uigizaji ili kufafanua maana
kama ilivyo pijini.
Sifa hizi zinazifanya krioli kuwa na hadhi ya lugha kama lugha zingine asilia
(zisizoibuka katika mazingira tuliyotaja) na hutumika rasmi katika elimu,
biashara, kuandika fasihi na hata huweza kuwa lingua franka. Mfano wa nchi
zinazotumia kirioli ni Sierra Leone, Liberia, Gambia, Hawii, na Mauritius.
Wanaisimu-jamii wengi wanasema kuwa dhana za kipijini na kikrioli ni mfano
bora wa jinsi binadamu wote, wanavyoweza kuutumia uwezo wao jumuishi
katika mazingira tofautitofauti.
Majedwali haya yanaeleza kwa muhtasari jinsi kirioli inavyoibuka.
63
1. Lugha za wazazi (Pijini)
Uwezo jumuishi
Lugha ya watoto (Kirioli)
2.
Pijini ya mama Pijini ya baba
Lugha finyu Lugha finyu
Mazingira
Kirioli (lugha ya watoto)
3. Pijini finyu 4 Pijini finyu
Kirioli Pijini Thabiti
(krioli ya Hawaii)
Kirioli
(Krioli ya Kiingereza ya
Torress Straits)
5 Pijini finyu
Pijini Thabiti
Pijini Pana Thabiti
64
Kirioli (Tok Pisini ya Papua New Guinea)
Kutokana na majedwali haya, inatudhihirikia kwamba, ili lugha yoyote ya pili
(kama Pijini) iwe lugha asili (ya mama) au kirioli, itabidi ifanyiwe marekebisho
fulani fulani na watumizi wake. Marekebisho yenyewe yatahusu kuondoa
upungufu wowote uliomo katika viwango vyote vya kiisimu fonolojia,
mofolojia, sintaksia na msamiati. Hapo ndipo lugha hiyo (kirioli) itakapoweza
kuwa chombo kiaminifu na kinachosadifu mawasiliano ya jamii husika katika
ngazi mbalimbali.
4.4 NADHARIA ZA ASILI YA PIJINI
Nadharia kadhaa zimependekezwa kuelezea asili ya pijini:
1. Nadharia mahsusi za lugha.
(a) Nadharia ya lugha ya kibaharia (nautical jargon)
(b) Nadharia ya lugha ya kitoto (baby talk)
2. Nadharia za kijumla.
(c) Nadharia ya uundaji upya leksimu (relexification)
(d) Nadharia jumlishi (universalist)
3. Nadharia zinazozingatia tofauti.
(e) Nadharia zenye kiini kimoja (common-core)
(f) Nadharia zenye safu msingi (substratum)
Hebu tuzifafanue nadharia hizi.
4.4.1 Lugha ya Kitoto.
Hii ni nadharia inayoshikilia kwamba pijini zilizuka kutokana na kuiga na
kurahisisha lugha aliyoisikia mtu. Hii ina maana kwamba, mtu anajifunza lugha
lakini hajifunzi lugha hiyo vyema. Kuna hata wataalamu, kama Hesseling (1933),
wanaodai kuwa pijini zilizuka kutokana na ujifunzaji makosa wa lugha uliofanywa
na watumwa.
65
Bloomfield (1933) anaeleza kuwa pijini ilizuka pale ambapo watu walijaribu
kuiga jinsi wenzao wasioifahamu lugha vizuri wanvyozungumza. Kwa mfano,
mwajiri (Bwana) anapozungumza na mtwana anairahisisha ile lugha yake na
kuiga lugha mbovu ya mtwana yule ili waelewane. Vivyo hivyo, mtu mzima
anapozungumza na mtoto ambaye bado hajaimudu lugha vizuri anairahisisha
lugha yake ili ilingane na ile ya mtoto. Basi mtwana anaposikia jinsi mwajiri
wake anavyozungumza anakosa kielelezo cha kuiga na anaiga lugha mbovu.
Nadharia hii basi inazo harakati mbili. Moja huanzishwa na wazungumzaji wa
lugha yenye hadhi ya juu ambao hurahisisha lugha yao. Ya pili, huanzishwa na
wazungumzaji wa lugha ya hadhi ya chini ambao hurahisisha lugha wanayoisikia
pale wanapojaribu kujifunza lugha hiyo. Katika hali ya kwanza, kikundi cha hadhi
ya chini kinaiga kinachosikia kutoka kwa kundi lenye hadhi ya juu. Katika hali ya
pili, kundi lenye hadhi ya chini ndilo huongoza katika kufanya makosa, na lile la
hadhi ya juu linaimarisha tu makosa hayo.
4.4.2. Lugha ya Kibaharia (Nautical jrgon theory)
Kwa mujibu wa nadharia hii meli zilizoabiri bahari zilikuwa na mabaharia
waliozungumza lugha na lahaja tofauti. Kwa hivyo ilibidi kuwepo na lugha moja
iliyoeleweka na mabaharia wote. Lugha hii iliyotumiwa na mabaharia
ikafahamika na Waafrika, Wazungu na Wahindi waliofanya kazi ya ubaharia.
Yamkini msamiati wa kibaharia ulikuwa kiini cha lugha hii, na lugha hii ilipanuliwa
kwa nyongeza kutoka kwa lugha za asili za mabaharia. Hii ndiyo sababu pijini na
krioli katika maeneo fulani ulimwenguni zitafanana, lakini zitofautiane na zile za
maeneo mengine.
Nadharia hii inapata msukumo kutokana na utafiti wa Todd (1990:33)
anayesema kuwa kuanzia karne ya 17 mabaharia walikuwa na lugha yao
mahsusi. Pia kuna msamiati wa kibaharia katika pijini nyingi duniani. Katika
Cameroon pidgin tunapata maneno kama:
66
Hib < heave sukuma
Kapsal < capsize pinduka
Manawa < man of war mtu wa vita
Reinecke (1937) alifanya utafiti na akakuta kwamba mabaharia waliozungumza
lugha tofauti katika meli moja waliunda msamiati mpya wanaoufahamu wote wa
maneno 300 katika kipindi cha miezi michache.
Ingawa tunakiri kwamba mabaharia walisambaza msamiati wa kibaharia katika
pijini mbalimbali ulimwenguni, nadharia hii haielezi kwa nini pijini zenye misingi
ya Kiingereza, Kifaransa, Kireno, na Kihispaniola zinafanana.
4.4.3.Asili moja (Monogenesis Theory)
Usuli wa nadharia hii ya asili moja ni kwamba pijini zote zinahusiana kinasaba na
zimetoka kwa proto-pijini au pijini-mame moja. Kwa hivyo, kule kufanana kwa
pijini kunaelezwa kuwa kunatokana na jadi moja (common ancestor) hapo
zamani.
Inafikiriwa kwamba hii proto-pijini inayozungumziwa katika nadharia hii ni pijini
ya Kireno ambayo labda ilikuwa ni mabaki ya lugha ya Sabir. Sabir ilikuwa lingua
franka ya zamani iliyotumiwa na wapiganaji wa Kikristo (crusaders) na pia kama
lugha ya kibiashara ya eneo la Mediterranean.
Nadharia hii inafafanua kwamba tofauti zinazopatikana katika pijini mbalimbali ni
matokeo ya kubadilisha msamiati kunakoendelea.Kulingana na nadharia hii,
kipijini cha Kireno ndicho kilikuwa msingi wa pijini nyingine ambazo ziliundwa
baadaye, lakini pijini hizi zilibadilisha msamiati wa pijini msingi na kutumia
msamiati kutoka kwa lugha nyingine huku zikihifadhi msingi wa kisarufi
unaofanana.
67
Njia hii ya kubadilisha msamiati wa lugha fulani huku ukihifadhi muundo wa
kisintaksia inajulikana kama uundaji upya wa leksimu (relexification).
Kwa hivyo nadharia hii inadai kuwa pijini na kirioli za Ulaya ni vibadala vya pijini
ya Kireno ya Karne ya 15 vilivyoundiwa msamiati mpya. Pijini hii mwanzo
ilitumiwa katika upwa wa Afrika na baadaye ikafika India na nchi nyinginezo za
Mashariki ya Mbali (Far East). Kwa njia hii, pijini zote za Ulaya zinahusiana
kupitia kwa mchakato wa kudumisha sarufi na kubadili msamiati.
4.4.4 Maendeleo Sambamba (Independent Parallel).
Msingi wa nadharia hii ni kwamba pijini na krioli zilizuka kila moja kivyake na
zikaendelea kukua sambamba kwa sababu zilitumia malighafi ya kiisimu
iliyofanana na zilikulia katika mazingira yaliyofanana.
Kwanza, lugha kuu za wazungu hazikuwa tofauti kimuundo. Vile vile lugha
nyingi za waafrika (watumwa) zilitokana na kikundi kimoja cha familia ya lugha
ambazo wanaisimu huzibainisha kama Lugha za Afrika Magharibi.
Hall (1961) alieleza kuwa ingawa lugha hizi zilizuka kila moja kivyake kulikuwepo
na maeneo machache ya mwingiliano kama inavyoonyeshwa hapa chini.
English Melanesian
(French n.k) (Chinese,
African n.k.)
4.4.5 Lugha ya hadhi ya chini (Substratum theory)
Mahlhausler (1986:119) anatoa wazo kwamba pijini huunganisha msamiati wa
lugha yenye hadhi ya juu (superstratum) na sarufi ya lugha ya hadhi ya chini
(substratum). Hii ina maana kwamba pijini ni lugha ya mseto.
68
Naye Romaine (1988:102) anadai kuwa sura mbalimbali za kifonolojia, kisintaksia
na kileksia, zinazopatikana katika pijini zimetokana na lugha za Kiafrika.
Wanazuoni wengi wanasema kuwa pijini na kirioli zina msingi wa Kiafrika.
Goodman (1964) ametoa hoja kwamba ni baada tu ya kukubali kuwa kirioli zote
zenye msingi wa Kifaransa zina asili yake Afrika Magharibi ndipo tutaelewa kwa
nini zinafanana.
Pijini na kirioli huzungumzwa hasa katika nchi za ulimwengu wa tatu.
Zinahusishwa sana na maswala ya kisiasa na kijamii. Kuna takriban pijini na
kirioli mia moja duniani. Pijini nyingi zina misingi yake katika lugha za Ulaya,
hususan Kihispania, Kireno, Kifaransa, Kiingereza na Kidachi. Kikundi kingine
kinachofuata kwa ukubwa kina misingi yake katika lugha za Kiafrika.
Zoezi
Kwa kuzingatia nadharia hizi, unafikiria Sheng ni pijini au kirioli. Toa sababu
zako.
4.6 HITIMISHO
Katika somo hili, tumeanza kwa kujadili swala la lingua franka na
tumeonyesha majukumu yake katika jamii. Vilevile tumeeleza na
kuonyesha jinsi zinavyotumika kama lingua franka. Pili, tumefafanua
dhana za pijini na kirioli na vilevile kuonyesha nadharia mbalimbali
ambazo zimetolewa na wanaisimu kuhusiana na swala la kuzuka
kwa lugha hizi..
69
Marejeleo Teule
Bickerton, D. (1971) Inherent Variability and Variable Rules. Foundations of
Language 7.
Bloomfield,L. (1933) Language. New York. Holt. Rinehart and Winston.
Chimera, R. (2000) Kiswahili: Past, present and Future Horizons. Nairobi.
Nairobi University Press.
Guthrie, M. (1967) The Classification of the Bantu Languages. London Dawsons
of Pall.
Mbaabu,I. (1978) Kiswahili Lugha ya Taifa. Nairobi: Kenya Literature Bureau.
Onyango, J.O. (2002) AKS 102: Historical Development of Kiswahili:Kiswahili
Module. Nairobi: Institute of Open Learning, Kenyatta University.
Polome, E.C. (1967) Swahili Language Handbook. Washington D.C. Centre for
Applied Linguistics.
Swaleh A. (1997) Lugha ya Kiswahili (ni) pijini au krioli? Makala
yaliyowasilishwa katika Idara ya Kiswahili. Chuo Kikuu cha Nairobi.
Todd, L. (1990) Pidgins and Creoles. Routledge.London.
70
SOMO LA TANO
UWILI LUGHA
5.0 Utangulizi
Katika somo hili tunanuia kuelezea maana ya uwili-lugha na ulumbi. Pamoja na
hayo, tutaonyesha athari ambazo hutokana na lugha mbili au zaidi kuwa pamoja.
Vile vile tutajadili swala la lugha rasmi, lugha ya taifa , diglosia na triglosia. Na
mwisho tutaangalia swala la utowekaji wa lugha katika jamii.
5.1 Madhumuni
Baada ya kulipitia somo hili, tunatarajia kwamba utaweza:
1. Kueleza maana ya uwili-lugha na kuonyesha athari zake.
2. Kueleza maana ya lugha rasmi na lugha ya taifa.
3. Kueleza kwa fasili dhana za diglosia na triglosia.
4.Kuonyesha sababu za utowekaji wa lugha na jinsi ya kuzilinda lugha hizi.
5.2 UWILI-LUGHA
Mtagusano wa wanajamii huzua hali ya uwili lugha katika jamii mbalimbali. Kwa
mujibu wa Bloomfiled (1933) uwili-lugha ni umilisi wa lugha mbili kama ule
alionao mzawa wa lugha moja katika lugha yake.
Haugen (1956) naye anaona kuwa uwili-lugha ni kitu ambacho huanza wakati
mzungumzaji wa lugha moja anapoweza kutoa kauli kamili na zenye maana
katika lugha nyingine.
Katika hali ya wingi lugha tunaweza kuzungumzia kuhusu mtu mmoja au
wanajamii wote au wengi kuwa wana wingi-lugha.
71
Mtaalamu Grosjean (1982:vii) anakadiria kuwa karibu nusu ya idadi ya watu
ulimwenguni huzungumza zaidi ya lugha moja. Naye Romaine (1989:6) anadai
kuwa hata zile nchi ambazo zinafikiriwa kuwa na lugha moja tu kama vile
Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zina wazungumzaji ambao ni wana uwili
lugha. Kwa mfano, utapata kuwa maeneo ya kimipaka, kwa mfano, Ufaransa,
kuna lugha hizi:-Breton, Flemishi, Occitan, na kadhalika. Mara nyingi watu
wanaopakana hujipata wakizungumza lugha ya jirani zao.
Zingatia
Katika somo hili tutatumia istilahi ya uwili- lugha kurejelea pia wingi
lugha
5.3 Sababu za kuwepo na Uwili lugha .
Kunazo sababu nyingi ambazo zinawafanya watu kuzungumza zaidi ya lugha
moja. Sababu hizi ni pamoja na:
1. Ndoa mseto
Hali ya ndoa mseto ni jambo la kawaida katika ulimwengu wa sasa. Hali hii
inapotokea mke au mume hulazimika kujifunza lugha ya pili.
2. Elimu
Aghalabu watu wanapoenda shuleni wanafunzwa lugha ya pili. Kwa mfano,
mtoto anapokuwa mdogo hujikuta katika mazingira ambayo wazazi wake
wanatumia lugha wenyeji. Anapotimia umri wa miaka sita, mtoto huyu hujiunga
na shule. Shuleni, hufunzwa Kiingereza na Kiswahili. Ripoti ya hivi karibuni
inaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi elfu mia nne wako katika nchi mbalimbali
kwa masomo ya juu. Wale walio katika nchi zinazotumia lugha nyinginezo kama
vile Kijerumani au Kifaransa hulazimika kujifunza lugha hizi hata kabla ya
kujiunga na vyuo hivyo.
72
3. Dini
Dini anayofuata mtu inaweza kuwa katika lugha fulani, kwa mfano, ikiwa dini ni
ya Kiislamu, utapata kwamba Waislamu wengi wanafahamu Kiarabu kwa sababu
hii ndiyo lugha ambayo hutumiwa sana katika mahubiri hasa kukariri korani.
Swali
Je, waweza kufikiria sababu zingine zinazomfanya mtu kutaka kujua zaidi
ya lugha moja?
5.4 Uchaguzi wa lugha katika jamii zenye uwili-lugha- Dhana ya
himaya
Tunapoangalia Afrika kwa mfano, tunaona kuwa mtu yeyote anayesafiri kwa
sababu za kiuchumi au kuhamia sehemu fulani kwa sababu mbalimbali huwa
mwana uwili lugha. Hata kama kuna wazungumzaji wa lugha moja tu, wengi
wa watu ni wana uwili-lugha, (Myers- Scotton 1993).
Tafiti nyingi ambazo zimefanywa katika jamii zenye uwili-lugha zimejihusisha na
tabia ya uchaguzi wa lugha wanaofanya wazungumzaji. Istilahi hii ya tabia ya
uchaguzi ni muhimu. Katika hali nyingi, wazungumzaji wanaweza kutumia
lugha zao wanapozungumza na wenzao. Ukweli ni kwamba, lugha fulani
huhusishwa na miktadha fulani. Kwa mfano, mandhari, mada na wahusika
katika mazungumzo hayo, Mesthrie (2000).
Mtaalamu Fishman (1967) katika kulishughulikia swala hili, alijihusisha na
kuonyesha ruwaza ya matumizi ya lugha. Aliibuka na dhana ya himaya
(domains) kama namna ya kuonyesha ruwaza hizi. Alidai kuwa katika jamii
yenye uwili-lugha, lugha mbalimbali huhusishwa na himaya tofauti za matumizi.
73
Mifano ya himaya hizi ni pamoja na familia, elimu, kazi au ajira, urafiki, utawala
wa kiserikali, n.k.
Hivyo basi katika himaya hizi, mtu atachagua mojawapo ya lugha anazozifahamu
ili kuzitumia. Kwa mfano, Myers Scotton (1992) amegundua kuwa katika bara la
Afrika, ruwaza ambayo inajitokeza kwa wingi ni lugha ya kwanza ya
mzungumzaji, pamoja na lingua franka ya wenyeji, kwa mfano, Kiswahili, kisha
lugha ya kigeni kama vile Kiingereza au Kifaransa.
Ruwaza ya matumizi ya lugha katika sehemu nyingi za Afrika zinategemea hali ya
kijamii ya mtu na aina ya muingiliano ambayo mtu hujihusisha nayo (Mesthrie
2002).
Zoezi
Kwa kuzingatia dhana ya himaya, onyesha namna marafiki zako
wanavyotumia lugha wanazozifahamu.
5.5 Mambo muhimu ya kuzingatiwa katika uwili-lugha
Mtaalam Makey (1962) anapendekeza mambo manne ambapo fasiri yo yote ya
uwili lugha inahitaji kuzingatia: kiwango, dhana, ubadilishaji na athari (au
uingiliaji).
(a) Kiwango
Tumeona kuwa mwana uwili-lugha ni mtu ambaye anazungumza lugha mbili kwa
ustadi.Kwa mfano, Bloomfied anadai kuwa mwana uwili-lugha anahitaji kuwa na
ustadi, katika lugha ya pili kama alionao katika lugha yake ya kwanza.
74
Tunapowasikia watu wakiongea, tunatanbua kuwa watu hawa hutofautiana
katika jinsi wanavyodhibiti lugha yao ya kwanza, na hali hii inawakumba wale
wanaojifunza lugha ya pili. Ni lini tunaweza kuamua kuwa sasa mtu
anazungumza lugha ya pili kama anavyozungumza lugha yake ya kwanza ?.
Hivyo basi swali tunalohitaji kujiuliza ni je, kwa kiasi gani mzungumzaji
anafahamu lugha hizo mbili au tatu?
Mtazamo tofauti na huu ni ule ambao unachukuliwa na wanaisimu ambao
hawatazami uwili-lugha kwa kuzingatia kiwango bali kwa kuzingatia dhima ya
lugha hiyo.
2. Dhima
Wana uwili-lugha huchagua lugha kulingana na kile watakachofanya na lugha
hiyo. Kwa mfano, uhusiano wao na watu wanaoongea nao na kile
wanachozungumzia. Ruwaza ya uwili-lugha hubadilika kila mara kulingana na
kazi itakayotendwa na lugha iliyochaguliwa kutumika.
Tuchukue mfano wa Mkenya ambaye ameishi Ujerumani kwa miaka mingi. Mtu
huyo anakifahamu Kijerumani, Kiingereza na Kiswahili. Sasa anaporudi
nyumbani na kwenda benki anafikiria kutumia Kiswahili. Lakini anatambua kuwa
hawezi kujieleza vilivyo kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu hajawai kuwa na
majadiliano ya aina hii kwa Kiswahili. Itambidi achague lugha nyingine ambayo
ni Kiingereza ili kuwasiliana na meneja.
Hii inamaanisha kuwa kuna hali nyingi ambazo wana uwili-lugha wanaweza
kujieleza vizuri kwa lugha moja kuliko katika lugha nyingine.
3. Uingiliaji
75
Kuna tajriba fulani katika maisha ambazo humfanya mtu aweze kujieleza vizuri
kwa lugha moja kuliko nyingine. Hii haimaanishi kuwa hawaielewi lugha hiyo,
La. Tatizo ni kwamba wao hujikuta kuwa hawalipati neno mwafaka ambalo
wanaweza kulitumia wanapozungumzia mada fulani. Weinreich (1953) anadai
kuwa uingiliaji ni ile hali ambayo ukiukaji wa kaida katika lugha hutokea katika
mazungumzo ya wana uwili-lugha kutokana na wao kujua zaidi ya lugha moja.
Uingiliaji unaweza kutokea katika viwango vyote. Kwa mfano, unaweza kuwa
katika kiwango cha fonetiki ambapo matamshi ya mtu yanakuwa kama yale
yanayopatikana katika lugha nyingine. Katika kiwango cha semantiki, mtu
huweza kushindwa kuchagua neno linalofaa. Ni rahisi kuona kuwa hata katika
kiwango cha kisantaksia uingiliaji huu hutokea hasa katika mpangilio wa maneno
katika sentensi.
4. Ubadilishaji
Katika hali hii tunaangalia kiasi ambacho mzungumzaji hubadili mazungumzo
kutoka kwa lugha moja hadi nyingine.
Zoezi
Ukirejelea Chacha L.M. na wengine (2002) AKS100: Introduction to the
Study of Language, onyesha athari mbali mbali za kiisimu zinazojitokeza
katika jamii yenye wingi lugha.
Kumbuka
Uwili lugha ni hali ambapo mtu anaweza kuzungumza lugha mbili. Wingi-lugha
ni hali ya mtu kuzungumza zaidi ya lugha moja.
76
Swali
1. Uwili lugha ni nini?
2. Fafanua dhana ya himaya katika swala la uwili lugha
3. Ni mambo gani tunahitaji kurejelea ili kujua viwango vya ufahamu vya
mzungumzaji fulani katika hali ya uwili lugha.
5.6 LUGHA RASMI NA LUGHA YA TAIFA
5.6.1 Lugha Rasmi
Hii ni lugha ambayo imeteuliwa katika nchi fulani ili itumiwe katika mawasiliano
yote rasmi katika nchi hiyo. Lugha hii huchaguliwa ili kutumiwa katika shughuli
za serikali, kwa mfano, afisini, kuzungumza na wageni, katika taasisi mbalimbali
na ndiyo hutumiwa kwenye vyeti na shahada.
Nchi nyingi zilizotawaliwa zinatumia lugha za waliokuwa watawala wao kama
lugha zao rasmi. Wakati mwingine baada ya nchi kupata uhuru, huamua
kutumia lugha ya humo nchini kama lugha rasmi. Kwa mfano, Kenya na Uganda
hutumia lugha ya Kiingereza kama lugha rasmi ilhali nchi ya Tanzania hutumia
Kiswahili kama lugha rasmi. Tunasubiri kuona jinsi lugha ya Kiswahli na
Kiingereza zitatumika iwapo katiba mpya itakubali kuwa Kiswahili kiwe pia lugha
rasmi nchini.
5.6.2 Lugha ya Taifa
Hii ni lugha ambayo kisiasa, kijamii na kiutamaduni inawakilisha watu fulani.
Viongozi wa nchi huchagua lugha ya taifa hasa wanapogundua kuwa lugha ni
kipengele muhimu katika utamaduni wa taifa (Chimera 2002). Hivyo basi lugha
77
ya taifa huwa ni lugha inayotambulisha na kutumiwa na taifa fulani. Lugha hii
huweza vile vile kuwaunganisha wananchi wa matabaka mbalimbali. Tukitazama
kwa mfano, viongozi wanaoshika hatamu, tunaona kuwa wanaweza kuchukuliwa
tu kama viongozi wa taifa zima bali sio wa makabila mbalimbali iwapo watatumia
lugha moja ya taifa.
Lugha ya taifa inaweza kulinganishwa na bendera ya taifa ya nchi.Vivyo hivyo
lugha huitambulisha taifa. Lugha ya taifa huwa na kusudi la kuibusha uzalendo
miongoni mwa watu, (Chimerah 2002).
Katika baadhi, ya nchi utapata kuwa lugha rasmi ndiyo pia lugha ya taifa ingawa
sio lazima mambo yawe hivyo. Kwa mfano, katika nchi ya Tanzania, Kiswahili ni
lugha rasmi na pia lugha ya taifa.
Kumbuka
Si lazima kila nchi iwe na lugha ya taifa ingawa ni lazima kila nchi iwe
na lugha rasmi.
Swali
Huku ukitoa mifano eleza maana ya lugha Rasmi na lugha ya Taifa.
5.7 DIGLOSIA NA TRIGLOSIA
Diglosia ni hali ya kuwepo kwa lahaja mbili za lugha moja, kila moja ikikidhi
mahitaji tofauti ya kijamii.
Kuna wataalamu wawili wa isimujamii walioifafanua dhana hii ya diglosia lakini
kwa misisitizo mbalimbali. Hawa ni Ferguson (1959) na Fishman (1967).
78
5.7.1 MAELEZO YA DIGLOSIA KAMA YANAVYOTOLEWA NA FERGUSON
Ferguson alitambua kwamba wazungumzaji hutumia vibadala tofauti vya lugha
katika miktadha tofauti. Alieleza kuwa kulikuwa na hali maalum ambapo
vibadala viwili vya lugha vinakuwepo ubavu kwa ubavu katika jamii fulani, kila
moja ya vibadala hivyo ikiwa na dhima mahsusi. Hali hii ndiyo aliyoiita diglosia.
Ferguson aliona kuwa hali hii ni tofauti na pale ambapo lugha sanifu na lahaja
nyingine ya lugha hiyo zilitumika, au pale ambapo lugha mbili tofauti zilitumiwa
katika jumuia lugha, kila moja ikiwa na dhima yake.
Ferguson aliifafanua dhana ya diglosia kupitia kwa vigezo tisa:
dhima (function)
fahari(prestige)
urithi wa fasihi (literary heritage)
upataji au ujifunzaji lugha (acquisition)
usanifishaji (standardization)
uthabiti/utangamano (stability)
sarufi (grammar)
leksimu (lexicon) msamiati
fonolojia (phonology)
(i)DHIMA
Dhima ndicho kigezo muhimu sana katika diglosia. Ferguson asema kuwa huwa
kuna vibadala viwili vya lugha hiyo moja, ambapo moja huwa ni lahaja ya Juu (J)
na nyingine ni lahaja ya Chini (CH). Katika Kiarabu, J ni lugha kielelezo ya kale
(Classical Arabic) ambayo ndiyo iliyotumiwa katika Korani, na CH hutumiwa
katika miktadha isiyo rasmi na ya kujiburudisha. Hapa kuna mifano:
79
Hali/Miktadha na uteuzi wa (J) au (CH) katika diglosia
Hali J CH
-Mahubiri kanisani au msikitini + _
-Maagizo kwa watumishi, wahudumu
hotelini, wafanyakazi, makarani _ +
-Barua (ya kirafiki) - +
-Hotuba bungeni + _
-Mhadhara katika Chuo Kikuu + _
-Mazungumzo kati ya marafiki x
-Matangazo ya habari x _
Lugha ya magazeti x _
(ii) FAHARI
Mielekeo ya wazungumzaji katika jamii zenye diglosia ni kwamba J ni bora,
yenye madaha, sanifu, na yenye mantiki zaidi. Inaaminiwa kwamba CH ni duni.
(iii) URITHI WA FASIHI
Kuna fasihi au maandishi mengi katika J ambayo yanafurahiwa na kuvutiwa na
jumuia lugha hiyo. Aghalabu utamaduni wa fasihi ya J huwa hauna msingi wake
katika jamii ya kisasa. Misingi yake ipo katika wakati uliopita au jumuia lugha
nyingine (Kifaransa, Kijerumani nk).
(iv) UPATAJI AU UJIFUNZAJI LUGHA
Katika diglosia, ujifunzaji wa lugha huwa tofauti kati ya kibadala J na CH. CH
itatumiwa kuzungumza na watoto, na pia kati ya watoto wenyewe; hivi kwamba
watu watafahamu CH bila juhudi za kimakusudi.
80
J huwa ni lugha ya ziada au ya pili ambayo watu hujifunza baada ya kuifahamu
CH. J hufahamika kupitia mafunzo ya shuleni. Hii ina maana kwamba wale
wanaojifunza J kamwe hawawezi kupata ufasaha kama ule wanaofikia katika CH.
Hii ni kwa sababu CH hutumiwa mara kwa mara katika mawasiliano ya kila siku
ilhali J hujifunzwa kwa kukariri (memorise) sheria za kisarufi.
(v) USANIFISHAJI
J ndiyo husanifishwa kwa kuwekewa mpangilio kamili. Makamusi, vitabu vya
sarufi, miongozo ya matamshi bora, na kwa ujumla vitabu vya matumizi sahihi ya
J huandikwa. Alfabeti na sheria za maendelezo katika J huwekwa.
Huwa hakuna uchunguzi wa kiusomi wa lahaja CH. Hata kuandika katika CH
huwa vigumu kwa sababu hakuna sheria za hijai zilizoimarika, na pia hakuna
anayetaka kuandika katika CH.
(vi) UTHABITI
Diglosia huwa ni hali iliyo thabiti na inaweza kudumu karne kadhaa. Ili lugha iwe
na zaidi ya lahaja au kibadala kimoja, sharti pawepo na diglosia katika lugha
hiyo. Mvutano kati ya J na CH katika diglosia hupungua kwa kiasi pale ambapo
kunatokezea mfumo wa lugha wa kati, unaochukua baadhi ya sifa za J na Ch. Ni
kawaida kwa CH kukopa maneno kutoka kwa J; lakini matumizi ya msamiati wa
CH katika J si jambo la kawaida.
(Viii) SARUFI
Ingawa J na CH ni maumbo ya lugha hiyo moja, huwa kuna tofauti nyingi kati ya
sarufi ya J na CH. Sarufi ya CH huwa sahili kuliko sarufi ya J.
(ix) MSAMIATI
Msamiati wa J na CH hutumiwa katika lugha zote mbili. Istilahi na msamiati wa
kiusomi hupatikana tu katika J. Katika CH kuna msamiati unaorejelea vyombo
81
vya nyumbani kama vifaa vya shambani, vyombo vya kupikia/jikoni nk ambavyo
havina vingine vinavyolingana navyo katika J.
Sifa ya kuvutia sana katika diglosia ni kuwepo kwa visawe (msamiati pacha)
ambapo CH na J kila moja zinachangia neno kwa dhana hiyo moja. Kwa mfano:
children - rasmi
kids - simo
baba - rasmi
buda - simo
Katika jamii zilizo na diglosia, mfumo wa J ndio unaowekwa katika maandishi na
wa CH ndio unaotarajiwa kuwa katika mazungumzo ya kila siku.
Swali
Toa mifano ya sifa hizi tulizozitaja za diglosia kulingana na hali
ya lugha nchini Kenya.
Ferguson alichukulia Diglosia kuwa ni hali thabiti ya lugha ambayo, pamoja na
lahaja za kimsingi za lugha hiyo, huwa na kibadala kilicho tofauti, cha hali ya juu,
na chenye mpangilio kamili.Kibadala hiki huwa na kusanyiko kubwa la fasihi
andishi lililotoka kwa jumuia lugha nyingine au kipindi cha awali cha lugha hiyo.
Huwa inafunzwa shuleni na kutumiwa katika maandishi mengi na mazungumzo
rasmi.Lakini hakitumiwi na kitengo cho chote cha jamii hiyo kwa shughuli za kila
siku.
82
HATIMA YA DIGLOSIA
Ferguson (1972:248) anaeleza kuwa diglosia huweza kuwa na hatima tatu
tofauti:
(a) itabakia thabiti kwa muda mrefu.
(b) katika hali fulani, shinikizo fulani zinaweza kusababisha kumalizika kwake.
Kwa mfano; ongezeko la watu waliosoma, kutanda kwa mawasiliano
katika nchi.
Watu wengi wanapoifahamu J na kutumia lugha ya kimaandishi kwa wingi,
matokeo yake yanakuwa ni kupungua kwa tofauti za kiisimu kati ya J na CH. Pia
kukua kwa utaifa kunakoambatana na tamaa ya kuwa na lugha ya taifa kama
ishara inayowaunganisha watu huchangia kumalizika kwa diglosia.
(c) J itakua na kuwa lugha au lahaja sanifu.
J inaweza kuwa sanifu ikiwa:
(i) tayari J ni lugha sanifu katika jumuia nyingine.
(ii) ikiwa jamii hiyo yenye diglosia itaungana na jamii hiyo nyingine.
5.7.2 DIGLOSIA KWA MUJIBU WA FISHMAN
Fishman (1967) anaamini kwamba tunahitaji kutofautisha kwa makini dhana za
diglosia na uwili lugha. Anasema kuwa uwili lugha ni swala linaloshughulikiwa na
wanasaikolojia na wanaisimunafsia; inarejelea uwezo wa mtu binafsi kutumia
zaidi ya vibadala au launi moja ya lugha (language variety launi za lugha
namna tofauti za matumizi ya lugha kutegemea mazingira, wakati, muktadha,
nk, k.v. lahaja, rejesta, nk). Diglosia hushughulikiwa na wanaelimujamii na
wanaisimujamii kulingana na dhima zake.
Fishman alibadilisha mapendekezo ya Ferguson kwa namna mbili:
1. Fishman hasisitizi sana umuhimu wa hali zilizo na vibadala viwili tu vya
lugha. Anaruhusu kuwepo kwa misimbo mingi tofauti inayoweza
kugawika katika makundi mawili: Juu na Chini.
83
2. Huku Ferguson (1972) akiona kuwa diglosia inachukua mstari wa kati wa
kiisimu (anasisitiza kwamba diglosia huwa na tofauti nyingi kuliko ilivyo
kati ya mitindo, na chache kuliko ilivyo baina ya lugha tofauti), Fishman
analegeza mipaka hiyo. Anaona kuwa diglosia haipo tu katika jamuia
zenye ulumbi ambazo kirasmi zinatambua lugha mbalimbali, na pia si
katika jumuia zinazotumia lugha wenyeji (vernacular) na lugha vielelezo
(classical varieties), lakini pia katika jamii zinazotumia lahaja tofauti, sajili,
au vibadala vya lugha vyenye dhima tofauti.
Fishman anatumia istilahi diglosia kurejelea kiwango cho chote cha tofauti za
kiisimu kuanzia kwenye tofauti ndogo za kimtindo katika lugha moja hadi kwenye
matumizi ya lugha mbili tofauti. Jambo muhimu ni kwamba tofauti hizo za
kiisimu ziwe zimetambuliwa na kupewa dhima tofauti katika jamii.
Uwili lugha humaanisha kuwa udhibiti wa J na CH unapatikana katika jamii yote.
Diglosia hurejelea mgawanyo wa dhima kati ya J na CH.
UHUSIANO KATI YA UWILI LUGHA NA DIGLOSIA
Diglosia
________________________________________
+ -
1. Diglosia na 2. Uwili lugha bila
uwili lugha diglosia.
Uwili lugha 3. Diglosia bila 4. Hakuna uwili lugha
uwili lugha wala ulumbi.
1. Diglosia na uwili lugha
84
Katika jumuia lugha kama hiyo karibu kila mtu atafahamu J na CH. Kwa mfano,
kule Paraguay, Guarani ni CH na Kihispania ni J. Kihispania ni lugha ya Kihindi-
Kizungu na Guarani ni lugha ya wenyeji wa Marekani.
2. Diglosia bila uwili lugha
Ili kuwa na hali kama hii, kunahitajika makundi mawili tofauti katika kitengo
kimoja cha kisiasa, kidini na kiuchumi. Kundi moja linakuwa la watawala na
linazungumza J pekee. Kundi la pili, ambalo ndilo kubwa, halina uwezo katika
jamii na huzungumza tu CH. Kwa mfano, barani Afrika, wakoloni walizungumza
Kiingereza huku wenyeji wakizungumza lugha zao.
Jumuia za kidiglosia zisizo na uwili lugha si jumuia lugha kwa sababu makundi
hayo mawili hayaingiliani kwa mawasiliano isipokuwa kwa kiasi kidogo sana
kupitia kwa wakalimani au kwa kutumia pijini.
3. Uwili lugha bila diglosia
Fishman anasema kuwa hali hii inarejelea jumuia ambazo zina wazungumzaji
wengi wenye uwili lugha, lakini hawatengi lugha hizo kwa miktadha au dhima
maalum. Lugha yo yote kati ya hizo inaweza kutumiwa kwa dhima yo yote.
Jumuia kama hizo huwa chache.
Uwili lugha bila diglosia hutokana na kuvuja kwa diglosia. Diglosia inayovuja
inarejelea hali ambazo, kibadala kimoja cha lugha kinavuja na kuchukua dhima
zilizokuwa zimetengewa kibadala kingine. Matokeo ya uwili lugha bila diglosia ni
ama kuzuka kwa kibadala kipya ambacho ni mchanganyiko wa J na CH, au moja
kuchukua mahali pa nyingine. Kwa mfano, huko Ubelgiji katika eneo
kunakozungumzwa Kijerumani, kuna mabadiliko ambapo watu wengi
wanazungumza Kifaransa (J) ingawa mwanzoni walizungumza Kijerumani (CH).
85
4. Hakuna Uwili lugha wala diglosia
Hali hii inahitaji kundi ndogo lililojitenga linalozingatia usawa
Jisajili kwenye:
Maoni (Atom)
isimujamii
SOMO LA KWANZA ISIMUJAMII 1.0 Utangulizi Katika somo hili tutatoa maana ya isimujamii pamoja na kueleza historia yake. Tutaeleza mikaba...
-
SOMO LA KWANZA ISIMUJAMII 1.0 Utangulizi Katika somo hili tutatoa maana ya isimujamii pamoja na kueleza historia yake. Tutaeleza mikaba...